Latest Posts

WAKILI INDIA ASHITAKIWA KWA KUNYWA BIA MAHAKAMANI KUPITIA MTANDAO, AOMBA MSAMAHA

Mahakama Kuu ya Gujarat, India, imeanza kusikiliza kesi dhidi ya wakili Bhaskar Tanna baada ya video iliyomuonesha akinywa bia na kuzungumza kwenye simu wakati wa kikao cha mahakama kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua mjadala mpana.

Video ya sekunde 15 iliyomuonesha Tanna akiwa katika kikao cha mtandaoni ilizua hasira miongoni mwa watumiaji wa mitandao na hatimaye kufikishwa mahakamani, ambapo Mahakama Kuu ilieleza kuwa kitendo hicho ni cha “matusi na cha kusikitisha”, kikionekana kuwa ni dharau kwa chombo cha utoaji haki.

Jaji wa Mahakama hiyo aliagiza hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya wakili huyo, akimtaka Msajili wa mahakama kutoa onyo rasmi na kumzuia Tanna kuendelea kuhusika katika kesi aliyoihudhuria kwa njia ya mtandao wakati tukio hilo lilipotokea.

Akijitetea mbele ya Mahakama, Tanna amekiri kuwepo kwa video hiyo lakini akasema ilikuwa ni kosa la kubonyeza kitufe kisicho sahihi. “Nilikusudia kutumia sauti lakini kwa bahati mbaya nilifungua kamera. Ilitokea baada ya usikilizwaji wa kesi, na nilizima video hiyo mara moja,” alisema.

Pamoja na maelezo hayo, Tanna aliomba msamaha bila masharti kwa majaji wote waliokuwepo katika kikao hicho, huku akisisitiza kuwa hakukusudia kuidhalilisha mahakama.

Kwa mujibu wa sheria ya kudharau mahakama ya mwaka 1971 nchini India, wakili anayekiuka maadili anaweza kuadhibiwa kwa kifungo kisichozidi miezi sita, faini, au vyote kwa pamoja.

Kesi hiyo imeahirishwa na inatarajiwa kuendelea kusikilizwa tena baada ya wiki mbili.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!