Latest Posts

WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI SABASABA WAPATA MSAADA WA VITABU NA UKARABATI WA MIUNDOMBINU

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Sabasaba iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara wamepata unafuu mkubwa wa vifaa vya kujifunzia baada ya shule hiyo kupokea vitabu 235 vyenye thamani ya shilingi 2,323,000/=, vilivyotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo.

Msaada huo umetolewa leo Januari 28, 2026 kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya uhaba wa vitabu uliokuwa ukiikabili shule hiyo, hususan vitabu vya masomo ya dini pamoja na vitabu vya rejea kwa ajili ya mazoezi, mitihani na kujipima kwa wanafunzi.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mwalimu Hassan Nyange, amewahimiza wanafunzi kutumia fursa hiyo kuongeza bidii katika masomo yao na kujiepusha na makundi hatarishi kama matumizi ya dawa za kulevya na unywaji wa pombe, akisisitiza kuwa shule ni msingi wa kujenga maarifa, ujuzi na nidhamu.

Mbali na msaada wa vitabu, Manispaa pia imetoa shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuanza ukarabati wa miundombinu ya shule, hatua inayotarajiwa kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa walimu na wanafunzi.

Kwa upande wake, Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo, Mwalimu Makala amesema kuwa msaada huo utaleta mabadiliko makubwa katika ufundishaji na ujifunzaji kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi waliokuwepo shuleni hapo, na ameahidi kuendelea kusimamia taaluma ili kuboresha matokeo ya kitaaluma.

Wanafunzi wa shule hiyo wameishukuru Manispaa kwa msaada huo wakisema vitabu hivyo vitawasaidia kufikia ndoto zao za kuwa wataalamu mbalimbali kama madaktari, wahandisi, wahasibu na walimu, na hivyo kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!