Latest Posts

WANASHERIA KENYA WAPINGA POLISI KUFICHA SURA KWENYE MAANDAMANO

Chama cha Wanasheria nchini Kenya (LSK) kimemkosoa vikali Waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen, kwa kutoa kauli inayopingana na uamuzi wa Mahakama Kuu uliopiga marufuku polisi kuficha utambulisho wao wakati wa maandamano.

Kauli hiyo ya Murkomen imetolewa Septemba 16, 2025, katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Citizen, ambapo alisema maagizo ya mahakama “yanaweza kutafsiriwa tofauti” na kwamba maafisa wanaweza kuficha utambulisho wao “ili kujilinda.”

“Agizo hilo linaweza kutafsiriwa kwa sababu hatutaruhusu maafisa wetu wa polisi kuhatarisha maisha yao kwa kuvaa sare wakati hawafai kuvaa sare,” alisema Murkomen.

Hata hivyo, Rais wa LSK, Faith Odhiambo, amejibu kwa ukali akisema kauli ya Murkomen inaonesha kutojua sheria, akisisitiza kuwa maagizo ya mahakama hayawezi kufasiriwa na mtu binafsi, taasisi au mamlaka yoyote isipokuwa mahakama za rufaa.

“Amri za mahakama ni za lazima, zinatekelezeka na lazima zifuatwe kikamilifu hadi pale zitakapoondolewa na mahakama yenye mamlaka. Hakuna uhalali wowote kwa afisa polisi kujificha wakati wa maandamano huku amri hiyo ikiendelea kutumika,” alisema Odhiambo.

Aliongeza kuwa iwapo polisi wataficha utambulisho wao, hatua hiyo itachukuliwa kama kitendo cha makusudi cha kudharau amri za mahakama.

Uamuzi wa Mahakama Kuu ulitolewa Agosti 2024, ukielekeza Inspekta Jenerali wa Polisi kuhakikisha maafisa wanavaa vitambulisho vya majina na namba za huduma wakiwa katika maandamano, na kwamba nyuso zao hazifunikwi ili kuhakikisha uwajibikaji na uwazi.

Sheria ya Jeshi la Polisi la Taifa (NPS Act) inatoa mwongozo kuhusu matumizi ya nguvu na namna maafisa wanavyopaswa kujilinda wakiwa kazini, ikisisitiza pia umuhimu wa kuzingatia misingi ya haki na utawala wa sheria.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!