Shirika la DSW kwa kushirikiana na TAHEA kupitia mradi wa unaolenga kujenga jamii imara, yenye uwezo, salama na inayostawi (REST) limeendesha mdahalo wa pamoja katika Kata ya Ifunda, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, uliolenga kutoa elimu kuhusu afya ya uzazi na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Mdahalo huo uliwahusisha wazazi, viongozi wa serikali pamoja na wanafunzi kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili.
Afisa Mradi wa REST katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Hidaya Juma amesema mdahalo huo ni sehemu ya mwendelezo wa utoaji wa elimu kwa jamii unaolenga kufikia kata mbalimbali zikiwemo Ifunda, Tanangozi, Kihorogota na Kising’a.
Akitoa elimu katika mdahalo huo, Mtendaji wa Kata ya Ifunda Happiness Mkongwa aliwataka wanaume kujitokeza kuripoti vitendo vya ukatili wanavyokumbana navyo ndani ya familia badala ya kuvifumbia macho.
Naye Afisa Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Hamis Sabuni amewahimiza vijana kuepuka kuwa chanzo cha ukatili wa kijinsia na badala yake wawe mstari wa mbele kuripoti matukio hayo huku akionya tabia ya kuyasuluhisha matukio ya ukatili ndani ya familia.
