Mamlaka nchini Marekani zimeeleza kuwa, watu wanne wameuawa baada ya mtu mwenye bunduki kufyatua risasi ndani ya kanisa la Mormon katika jimbo la Michigan lililopo katikati mwa Magharibi ya Marekani.
Tukio hilo limetokea Jumapili Septemba 28, 2025, ambapo watu wanane wameripotiwa kujeruhiwa vibaya, mmoja wao akiwa katika hali mbaya zaidi.
Taarifa ya Polisi imeeleza kwamba mtuhumiwa huyo aligonga mlango wa mbele wa kanisa kwa gari lake kabla ya kuanza kufyatua risasi kwa kutumia bunduki na kisha akalichoma jengo hilo moto wakati mamia ya watu wakiwa kanisani wakati huo.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Mkuu wa Polisi wa Grand Blanc, William Renye, alieleza kwamba mshambuliaji huyo aliuawa na polisi katika eneo la maegesho ya magari dakika nane tu baada ya tukio kuanza.
Mhalifu huyo ametambuliwa kuwa ni mwanajeshi wa zamani wa majini wa Marekani mwenye umri wa miaka 40, anayetoka mji jirani wa Burton, na Renye amesema kuwa wachunguzi watapekua nyumbani kwa mtuhumiwa huyo ili kuchunguza rekodi za simu yake na kubaini sababu iliyompelekea kufanya kitendo hicho.
Baada ya tukio hilo, Rais wa Marekani Donald Trump alishutumu shambulio hilo akisema ni shambulio lingine lililolenga Wakristo.
”Mshukiwa amekufa, lakini bado kuna mengi ya kujifunza. Hili linaonekana kuwa shambulio jingine lililowalenga Wakristo nchini Marekani,” Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social.