Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limefanikiwa kuwakamata watu watatu kwa tuhuma mbalimbali za mauaji na ukatili wa kijinsia, katika matukio tofauti yaliyotokea maeneo tofauti mkoani humo.
Akithibitisha tukio hilo Januari 6, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Alex Mkama ameeleza kuwa mtuhumiwa wa kwanza ni Helakimu Joseph Kacheli (50), mkulima na mkazi wa kijiji cha Sesenga, ambaye alikamatwa Januari 4 kwa tuhuma za mauaji ya mkewe Sofina Alipisini (27), mkazi wa Lumbachini. Inadaiwa kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi. Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alijaribu kujiua kwa kujikata koromeo kwa kutumia silaha kali, lakini aliokolewa na kwa sasa anapatiwa matibabu akiwa chini ya ulinzi wa Polisi.
Katika tukio jingine, Justine Bernad Thomas (42), mkazi wa kijiji cha Sogeambe, alikamatwa Januari 5 kwa tuhuma za kumuua Machafu Magembe Masanja (42) kufuatia ugomvi uliotokana na mzozo wa mauzo ya mpunga bila ridhaa ya marehemu.
Aidha, tukio la tatu linamhusisha Andrew Joseph Katanga (33), mkazi wa Katindiuka, Wilaya ya Kilombero, ambaye alikamatwa kwa tuhuma za kumbaka na kumlazimisha mwanawe wa miaka 14 . Tukio hilo lilitokea Desemba 31, 2025 baada ya mtoto huyo kudaiwa kufungiwa chumbani na kulazimishwa ngono.