Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema linawashikilia watu watatu kwa mahojiano, kufuatia tukio la kushambulia usafiri wa mwendokasi.
Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Murilo, Oktoba 1 mwaka huu, ikibainishwa kwamba baadhi ya mabasi yalirushiwa mawe katika maeneo ya Gerezani Kariakoo, Magomeni Mapipa, Magomeni usalama na Magomeni Kagera, tukio liliopelekea vioo vya mabasi hayo kuvunjika.
Aidha Jeshi hilo limesema chanzo cha matukio hayo kinafuatiliwa, ambapo pia watuhumiwa wengine waliohusika na tukio hilo wanatafutwa.
Hayo yanajiri wakati hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii, baadhi ya wananchi wa jiji hilo wameonekana wakihangaika kupata usafiri huo wa mwendo kasi, huku wengine wakijazana kwa mabasi machache yanayotoa huduma.
Aidha Serikali ilishasema suala la mwendokasi linatafutiwa ufumbuzi, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mabasi mapya, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya mabasi hayo katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.