Serikali Wilayani Tabora mkoani Tabora imewaunganisha zaidi ya watoto 20 waliokuwa wakiishi au kuzurura mitaani wakiombaomba bila sababu za msingi, licha ya kuwa na umri wa kwenda shule,ambapo watoto hao wamepelekwa kwenye vituo vya kulelea watoto wenye mahitaji maalum wakiwemo yatima, huku wengine wakiunganishwa na familia zao ili waweze kupata malezi bora pamoja na fursa ya elimu.
Akizungumza wakati wa ziara katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Igambiro kilichopo Kata ya Misha, Manispaa ya Tabora, Mkuu wa Wilaya ya Tabora ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Wilaya hiyo, Bi. Upendo Wella, amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha watoto wote wanapata haki zao za msingi.

Bi. Wella, aliyekuwa ameambatana na Wajumbe wa kamati hiyo, ameeleza kuwa kati ya watoto hao, sita wamepelekwa katika vituo vya kulelea watoto wenye mahitaji maalum, huku watoto 15 wakiunganishwa na wazazi au walezi wao ili waendelee kupata malezi stahiki.
Aidha, baada ya kukabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwemo chakula kwa watoto hao, Bi. Wella amewahimiza watoto kusoma kwa bidii, kuzingatia maadili mema na kujituma ili waweze kufikia ndoto zao na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wao, viongozi wa kituo hicho wameshukuru kwa msaada uliotolewa na kuahidi kuendelea kuwalea watoto hao katika mazingira bora, huku watoto wakiahidi kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao, sambamba na matarajio ya wadau wanaowaunga mkono.
