Watumishi wapya wa ajira zaidi ya 300 katika Manispaa ya Mtwara Mikindani wameelekezwa kujitahidi kuepuka kuwa chanzo cha migogoro katika jamii watakazokwenda kuzihudumia kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya utumishi wa umma.
Maelekezo hayo yametolewa leo Februari 10, 2026 na Naibu Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, Somwana Manjenga, wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa watumishi wapya 321 wa Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara ambapo watumishi hao wameajiriwa kati ya Januari 2025 na Februari 2026, na mafunzo hayo yanafanyika katika Chuo cha MUST, zamani TTC Kawaida.

Manjenga amesema watumishi wa umma wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayowaongoza pamoja na kufuata maelekezo yatakayotolewa na Serikali na kusisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufikia malengo ya Manispaa, ikiwemo kuongeza makusanyo ya mapato kutoka shilingi bilioni 7 zinazokusanywa kwa sasa hadi kufikia shilingi bilioni 10 kwa mwaka.
Ameeleza kuwa utoaji wa huduma kwa wananchi unapaswa kuzingatia uadilifu wa hali ya juu, uwajibikaji na weledi, akibainisha kuwa kutokuzingatia misingi hiyo kunaweza kusababisha changamoto katika jamii wanazozihudumia.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mtwara, Wakili Richard Mwalingo, amesema mafunzo elekezi ni msingi wa kazi kwa watumishi wapya na ni sehemu ya kuwaandaa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma na amewataka kuzingatia miiko ya kazi, kutii maelekezo sahihi ya viongozi na kufanya kazi kwa bidii.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mwalimu Hassan Nyange, amesema masuala ya fedha za kujikimu na masilahi ya watumishi yanafuatwa kwa mujibu wa taratibu, huku akieleza kuwa madeni ya watumishi yatalipwa kwa kuzingatia miongozo iliyopo.
