Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga ameagiza kurekebishwa mara moja kwa makosa yaliyofanyika katika ujenzi wa jengo la kanda la Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Jijini Mwanza, ambayo yamesababisha mradi huo kuchelewa kukamilika kwa wakati uliopangwa.
Waziri Kapinga ametoa agizo hilo Januari 5, 2026 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo la TBS kanda ya Ziwa, lililopo jijini Mwanza.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetoa zaidi ya Sh. Bilioni 12 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, hivyo ucheleweshaji wake unapunguza kasi ya utekelezaji wa mipango ya serikali.
Kapinga ameongeza kuwa kuanzia sasa, makosa yote yaliyofanyika yarekebishwe na sababu zilizotolewa na Mshauri hazikubaliki na zitakazokubalika ziwe zile zilizo nje ya uwezo wa Serikali hivyo hakuna budi kumsimamia mkandarasi ipasavyo.

Aidha, Waziri Kapinga amesema maono ya Rais Samia kuhusu kujenga Tanzania ya viwanda yanaanza na udhibiti wa ubora wa bidhaa, jukumu ambalo TBS ina nafasi kubwa ya kulitekeleza ambapo kwa kuzingatia hilo wameanza kwa kasi kubwa kujenga ofisi za kanda, ikiwemo hii ya Kanda ya Ziwa, pamoja na Dodoma ambako ujenzi umefikia karibu asilimia 90, na Arusha.
Amebainisha kuwa kukamilika kwa Ofisi hizo ni kuchochea dhamira ya Serikali chini ya Rais Samia kuweka mkakati wa siku 100 wa kutenga fedha ili vijana wapate ajira hivyo vijana wa Mwanza na maeneo ya Kanda ya Ziwa wanaofanya ujasiriamali wamalize shida zao katika kituo hicho
Amesema kukamilika kwa ujenzi kwa wakati kutasaidia kuboresha ubora wa bidhaa, kupunguza gharama za usafirishaji, kurahisisha upatikanaji wa huduma, na kupunguza hali ya wananchi kukata tamaa.

Aidha, amemtaka mshauri mwelekezi kushirikiana kwa karibu na mkandarasi kwa kuweka ratiba madhubuti ya utekelezaji, ili kuhakikisha mradi unasimamiwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt.Ashura Katunzi amesema ili kuendana na kasi ya Serikali katika utoaji huduma za viwango na ubora, kila mwaka shirika hutenga bilioni 3 kununua vifaa vya maabara ili ofisi hizo zitakapokamilika kuanza kazi mara moja.
