Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ameeleza kuwa diplomasia ya Tanzania imepita katika mtihani mzito zaidi tangu uhuru kufuatia matukio ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, lakini sasa nchi imerejea katika mstari baada ya kueleweka kimataifa.
Akizungumza leo, Januari 15, 2026, mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania katika hafla ya ‘Diplomatic Sherry Party’, Ikulu Chamwino, Balozi Kombo amekiri kuwa matukio ya uchaguzi uliopita yaliharibu taswira ya nchi duniani na kuzua maswali mengi kutoka kwa washirika wa maendeleo.
“Nilipokea simu nyingi na ujumbe wa maandishi wa kutia moyo na mshikamano kutoka kwa marafiki na washirika wetu wengi wa karibu. Baadhi walijumuisha wasiwasi pia, huku wengine wakiuliza nini kimeipata Tanzania, nchi inayojulikana kama kitovu cha amani kwa miaka 64 iliyopita katika kanda hii tangu uhuru wake. Wengine waliwasilisha ujumbe wao kupitia njia za kidiplomasia kwako Mheshimiwa, huku baadhi isivyo bahati wakitumia majukwaa na maeneo yasiyo rasmi”, amesema Balozi Kombo.
Waziri huyo amebainisha kuwa chini ya maelekezo ya Rais Samia, Wizara ilifanya kazi ya ziada kufafanua ukweli wa mambo kwa kutumia ushahidi katika miji mikuu ya dunia hatua iliyosababisha nchi kueleweka. Amesema kuwa Umoja wa Mataifa (UN) umekubali kutoa nafasi ya uponyaji kupitia Tume ya Uchunguzi (Inquiry Commission) iliyoundwa na Rais, ambayo itafuatiwa na mchakato wa maridhiano ya kitaifa.
Balozi Kombo amesisitiza kuwa mbinu ya “4R” (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya) ya Rais Samia imekuwa nguzo muhimu katika kurejesha imani ya jumuiya ya kimataifa, huku akibainisha kuwa kila sauti ya upinzani au wasiwasi ilisikilizwa na kufanyiwa kazi kwa wakati muafaka.
Hafla hiyo ya kuanza kwa mwaka mpya wa kidiplomasia imehudhuriwa na wakuu wa mashirika ya kimataifa na mabalozi wote, ikiashiria kuanza kwa ukurasa mpya wa ushirikiano baada ya kipindi cha msukosuko wa kisiasa mwishoni mwa mwaka jana.