Latest Posts

WAZIRI NDEJEMBI AZINDUA RASMI MITA JANJA ZA TANESCO, ASEMA NI HATUA KATIKA KIHISTORIA YA MAGEUZI YA SEKTA YA NISHATI

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, ameongoza uzinduzi rasmi wa Mita Janja (Smart Meters) za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), teknolojia mpya ya kisasa inayolenga kuongeza ufanisi wa usambazaji wa umeme na kuboresha huduma kwa mamilioni ya watumiaji nchini. Uzinduzi huo umeelezwa kuwa hatua ya kihistoria katika mageuzi ya sekta ya nishati nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika leo Ijumaa Desemba 05, 2025, Waziri Ndejembi amesema TANESCO imefikia hatua kubwa ya kimapinduzi katika kuboresha huduma kwa wananchi na kuongeza uwazi kwenye matumizi ya umeme.

Amesema uzinduzi huo unathibitisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika, wa kisasa na unaoendana na mahitaji ya teknolojia ya sasa.

Waziri Ndejembi amekumbusha changamoto nyingi zilizokuwa zikiwakumba watumiaji wa umeme kupitia mita za zamani, ikiwemo kushindwa kuona matumizi ya umeme kwa wakati halisi, ugumu wa kupanga bajeti, hitilafu za tokeni kushindwa kuingia na matatizo ya rimoti kuharibika au kupoteza kumbukumbu. Alisema baadhi ya wateja walilazimika kupanda ngazi au stuli ili kufikia mita zilizowekwa maeneo magumu, jambo lililoongeza usumbufu hasa wakati wa dharura.

Kupitia Mita Janja, wateja wataweza kuingiza umeme popote walipo bila kufika nyumbani, kufuatilia matumizi kwa muda halisi kupitia mfumo wa kidijitali na kupata taarifa za kuisha kwa umeme kwa wakati. Waziri Ndejembi alisema teknolojia hiyo itaongeza ufanisi kwa TANESCO kwa kurahisisha kubaini wizi wa umeme, kutambua uharibifu wa mita na kupunguza upotevu wa nishati kwa wakati halisi, hatua itakayoongeza mapato ya shirika na kuimarisha usimamizi wa rasilimali.

Ameendelea kwa kusema kuwa, TANESCO imeanza kufunga mita hizo katika maeneo mbalimbali nchini na kwamba wateja wa mwanzo waliopatiwa Mita Janja wameanza kutoa mrejesho mzuri, hatua ambayo imeongeza hamasa ya serikali na wadau kuimarisha utekelezaji wa mradi huo muhimu.

Waziri Ndejembi pia ameelezea maboresho mengine ya kiteknolojia ndani ya TANESCO yanayoendelea kutekelezwa, ikiwemo mfumo wa kisasa wa maombi ya umeme (Nikonekt), kituo kipya cha huduma za simu kwa wateja (Unified Call Centre) na matumizi ya chatbot ya JISOti inayorahisisha utoaji wa taarifa na huduma kwa wateja ambapo amebainisha kuwa, kutokana na idadi kubwa ya wateja zaidi ya milioni 5.6 mabadiliko hayo yatafanywa kwa awamu kulingana na mpango wa shirika.

Katika hotuba yake, Waziri huyo wa Nishati ameelekeza TANESCO kusambaza Mita Janja katika mikoa yote bila kuchelewa na bila gharama kwa wateja wenye uhitaji wa haraka, kuhakikisha wateja wapya wote wanawekewa mita hizo, kufanikisha ufungaji kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mfumo huo pamoja na kuboresha mfumo wa uendeshaji wa Mita Janja kila mwaka ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

Aidha, ameitaka TANESCO kuimarisha mawasiliano na kuongeza ubunifu katika utoaji wa huduma, akisisitiza kuwa Watanzania wanahitaji umeme wa uhakika na huduma bora zinazokidhi kasi ya mahitaji ya uchumi na maendeleo ya nchi.

Katika hatua nyingine, Waziri Ndejembi ameipongeza Bodi ya TANESCO, Menejimenti, wataalam wa TEHAMA na vitengo mbalimbali vilivyohusika katika utafiti, majaribio na uwekezaji wa mradi wa Mita Janja kwa zaidi ya miaka 18, akisema wameandika historia mpya katika mageuzi ya usimamizi wa umeme nchini na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa teknolojia hiyo ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na mfumo thabiti, wa kidijitali na wa kisasa wa usimamizi wa nishati.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!