Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, ametoa wito kwa vijana na wananchi wa Tanzania kulinda amani na kuepuka kushiriki maandamano, akisisitiza kuwa taifa bado linakabiliwa na athari nzito zilizosababishwa na maandamano ya Oktoba 29, 2025.
Amesema hayo usiku wa Novemba 28, 2025 katika burudani ya amani iliyofanyika Soko la Nyama Choma Kumbilamoto katika kata ya Vingunguti wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam akibainisha kuwa maandamano hayo yalisababisha vifo, uharibifu wa mali za serikali na binafsi pamoja na kusimama kwa shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Simbachawene ameonya kuwa kuna taarifa za mipango ya maandamano mapya yanayotarajiwa kufanyika Desemba 9, 2025, akisisitiza kuwa Serikali haitaruhusu kutokea kwa vurugu nyingine na kuwaomba wananchi ‘kutotumika na kuchochewa kurudia makosa yaliyopita’.
Akirejea athari za maandamano ya Oktoba 29, Waziri Simbachawene amewataka vijana kufahamu gharama kubwa za uharibifu wa miundombinu, ikiwemo kuchoma vituo vya mabasi ya mwendokasi- mradi alioutaja kuwa umejengwa kwa ajili ya wananchi wasio na uwezo wa kumiliki magari. Amefafanua kuwa miradi hiyo inagharimiwa na kodi pamoja na mikopo ambayo vizazi vijavyo vitapaswa kuilipa.
Akizidi kusisitiza umuhimu wa amani, Waziri Simbachawene amesema Tanzania inaonekana kuonewa wivu kutokana na mafanikio yake, hivyo wananchi wanapaswa kuepuka kuvuruga misingi ambayo imeijengea nchi heshima na utulivu wa miaka mingi. Ameongeza kuwa baadhi ya majirani wa Tanzania wamekumbwa na migogoro kwa muda mrefu, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kujifunza kutokana na changamoto za mataifa hayo.
“Na leo hii nilikuwa na mkutano mkubwa sana wa utatu kati ya Tanzania, Burundi na UNHCR (Shirika la kuhudumia wakimbizi duniani), tunafikiria namna ya kuwarudisha wakimbizi wale wa Burundi kurudi kwao maana wamekaa hapa karibu miaka 40…sasa tunafikiria warudi kwao kwa sababu masharti ya ukimbizi yameisha hawataki kuondoka, tunafikiria kutumia ushawishi wa nguvu ili waweze kuondoka. Kama wakimbizi hawataki kuondoka kwetu halafu sisi hatuienzi na kuiheshimu amani ya nchi yetu tutakuwa sisi ni wajinga wa mwisho kwa sababu tunaona na kusikia kwa wenzetu kinachotokea”, ameeleza.
Katika hatua nyingine, Waziri pia amewasisitiza wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi, akisema polisi ni sehemu ya jamii na wana jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao.
“Kazi kubwa niliyopewa ni kuhakikisha nyinyi wananchi mnakuwa wa kwanza kulinda usalama wenu na mali zenu, nyuma yenu liko jeshi la polisi la vijana wenu, watoto wenu kaka zenu, ndugu zenu, wanalinda amani yenu. Shirikianeni na jeshi la polisi, Jeshi la polisi na wananchi ni familia moja kwasababu kazi ya jeshi la polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zake, polisi wawe marafiki zetu…ni marafiki zetu sio marafiki zetu? polisi ni watoto wetu sio watoto wetu? Ni ndugu zetu sio ndugu zetu? Tusigombanishwe na polisi, Polisi ni marafiki zetu na nimewaambia polisi, sasa tunataka tuoneshe aina ya jeshi la polisi ambalo linajenga urafiki na wananchi”, ameeleza.