Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Malawi baada ya kutamatika kwa zoezi la kupiga kura kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani watakaounda serikali ya taifa hilo linalokabiliwa na mdororo wa uchumi.
Wastani unaonesha kuwa wapigakura milioni 3.7 walipiga kura licha ya uwepo wa taarifa za zoezi hilo kuchelewa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura ikiwa ni pamoja na changamoto ya udhibitisho wa alama za vidole.
Hata hivyo licha ya changamoto zote zilizojitokeza tume nchini humo imesema zimetatuliwa ili kuwaruhusu wapiga kura kutimiza haki yao kwa mujibu wa sheria za Taifa hilo.
Tume ya Uchaguzi nchini humo ina muda hadi Septemba 24 mwaka huu wa kuandaa na kuyatangaza matokeo kamili ya uchaguzi huo uliofanyika Septemba 16, 2025.
Rais wa sasa Lazarus Chakwera anatazamia awamu ya pili katika uongozi wa nchi hiyo huku akishindana na Rais wa zamani Peter Mutharika ambapo wote kwa pamoja wanajipigia chapuo kwamba watafufua uchumi wa nchi hiyo na kuongeza ajira zaidi hasa kwa vijana.
Hata hivyo licha ya washindani hao wawili kutazamwa Zaidi, bado wapo washindani wengine wapatao 15 akiwamo mwanamke pekee ambaye amewahi kuwa mkuu wa nchi Joyce Banda na wengineo.