Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limefanikiwa kumkamata Shabani Hassan Nalyoto (20), mkazi wa Kivukoni, Wilaya ya Kilombero, akiwa na silaha aina ya gobole na maganda saba ya risasi aina ya shotgun.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Oktoba 17, 2024, katika eneo la Muhola, Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.
Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema mtuhumiwa alikuwa akitafutwa kwa matukio mbalimbali ya uhalifu, ikiwa ni pamoja na ujangili. Wakati wa kukamatwa, Nalyoto alikutwa na nyara mbalimbali za serikali, ikiwamo nyama ya kongoni, sikio, na mkia wa mnyama tembo. Hii ni sehemu ya jitihada za kuzuia ujangili na uhalifu katika mkoa huo.
Katika tukio jingine, polisi wamemkamata Exavery Gampunje Mnyawanu (67), mkulima mkazi wa Uleling’ombe, akiwa na silaha aina ya gobole isiyokuwa na namba za usajili, risasi 13, pamoja na gramu 15 za baruti.
Mtuhumiwa alikuwa akimiliki silaha hiyo bila kibali, na inadaiwa alikuwa akiitumia kwa ajili ya uwindaji haramu. Tukio hili lilitokea Oktoba 19, 2024, asubuhi, katika kitongoji cha Ibumu, kata ya Uleling’ombe, Wilaya ya Kipolisi Ruhembe, mkoani Morogoro.
Aidha, Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limefanikiwa pia kuwakamata watu wawili, Ramadhani Selemani Pangala (38), mkazi wa Temeke, Dar es Salaam, na Acley Aloyce Mda (52), mkazi wa Manyoni, Singida. Watuhumiwa hao walikutwa wakiwa na nyara za serikali, zikiwemo vipande vitatu vya meno ya tembo, ambavyo walikuwa wakijaribu kuvisafirisha. Tukio hili lilitokea jioni ya Oktoba 18, 2024, katika kata ya Kasiki, Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.
Kwa upande mwingine, Jeshi la Polisi limeendesha oparesheni ya kukamata madereva waliofanya makosa hatarishi barabarani. Katika oparesheni hiyo, jumla ya madereva 34 walikamatwa na leseni zao kufungiwa. Kamanda Mkama alieleza kuwa, kati ya makosa yaliyowapelekea madereva hao kukamatwa, sita walikamatwa kwa kuendesha magari wakiwa wamelewa, 10 walikamatwa kwa mwendo kasi na hatarishi, huku wengine 18 wakikamatwa kwa makosa mengine ya usalama barabarani.