Latest Posts

MAHAKAMA YAZUIA WAMAASAI KUHAMISHWA, KUFUTIWA VIJIJI NGORONGORO

Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani Arusha kimezuia utekelezaji wa amri ya Serikali ya kufuta vijiji, kata na vitongoji vya tarafa ya Ngorongoro mkoani humo pamoja na kusitisha tangazo la kuwataka wananchi kuhama Ngorongoro.

Uamuzi huo wa mahakama umetolewa siku ya Alhamisi Agosti 22, 2024 na Jaji Mwenda wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha katika kesi namba 59630 ya mwaka 2024 kufuatia shauri la Isaya Oleposi, la kuiomba mahakama ipime na kutazama uhalali wa amri ile na kama ilitolewa na mtu mwenye mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.

Akizungumza nje ya mahakama hiyo, Wakili wa kujitegemea Peter Njau ambaye alimwakilisha Isaya Oleposi amesema kuwa amri ya mahakama imeambatana na amri nyingine ikiwamo shauri hilo kusikilizwa rasmi tarehe 26 Septemba, 2024 ambapo mahakama itaweza kuona kama amri iliyotolewa na serikali kupitia tangazo la Serikali namba 673 ya 2024 kama ni halali au siyo halali

“Kupitia maamuzi yaliyotolewa na Jaji Mwenda katika Mahakama Kuu ya Arusha, amri ile itakwenda kusimama kwa sababu kilichotolewa mahakamani leo hii ni zuio, amri ile imesimamishwa utekelezaji wake mpaka pale amri ya mahakama itakavyosema vinginevyo, na zuio hili limetolewa ili liweze kupisha usikilizwaji wa maombi mama ambayo ni ya kuweza kuona kama ile iliyotolewa ilikuwa halali au la”, ameeleza Wakili Njau.

Aidha amesema kuwa mteja wake na wakazi wengine wa Ngorongoro wanahisi kuwa aliyetoa amri ile hakuwa na mamlaka stahiki ya kuweza kutoa amri na wala amri yenyewe haikuwa halali.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!