Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Gilead Teri amesema mkoa wa Njombe una sifa kubwa ya uwekezaji na kuwa moja ya mikoa inayoongoza kwa wawekezaji wa ndani hali iliyosababisha watu wa mkoa huo kuwa na kipato kikubwa kinachofikia wastani wa Shilingi milioni tatu kwa mwaka kwa mtu mmoja.
Teri ameeleza hayo wakati akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa ofisini kwake ambapo amesema TIC imesajili miradi sitini na moja kwa mkoa wa Njombe ambapo mpaka sasa wawekezaji wamewekeza zaidi ya Dola bilioni tano za Kimarekani ambazo zinakaribia Trilioni kumi na tatu za Kitanzania huku zikitengenezwa ajira takribani elfu ishirini kwa mkoa huo.

“Watu wa Njombe wana kipato kikubwa wastani wa takribani milioni tatu kwa mwaka na mitaji hiyo ambayo wanayo wamewekeza kwenye maeneo mbalimbali nchini, mnafahamu pale Kariakoo na maeneo mbalimbali ni wafanyabiashara na wawekezaji wa Njombe, niwapongeze sana watu wa Njombe kwa kuwa na hii sifa kubwa lakini pia Njombe ni sehemu sahihi kwa wawakezaji wa nje ambao wanakuja hapa”, amesema Gilead Teri.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka ametoa wito kwa TIC kushirikiana na serikali ya mkoa wa Njombe katika jitihada za kuwakaribisha wawekezaji kwenye uwekezaji mkubwa wa hoteli za kisasa kwa kuwa Njombe imekuwa na kivutio cha pekee cha utalii wa baridi jambo litakalowafanya Watanzania kufika Njombe kupumzika hususani wakiwa likizo.
“Njombe ni sehemu ambayo wawekezaji wanaweza wakawekeza hoteli kwa ajili ya watu kuja kutulia, watu wengi sana wanaona labda utalii ni lazima waende Arusha kwa hiyo niombe TIC muiweke Njombe kama ni sehemu nzuri kwa ajili ya mapumziko na kupata baridi”, amesema Kissa.

Aidha katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa TIC amefanikiwa kutembelea baadhi ya wawekezaji ikiwamo kiwanda cha TANWAT kinachojihusisha na uzalishaji wa bidhaa za aina mbalimbali kutoka kwenye mazao ya misitu na kiwanda cha Oresco food Product ambao ni wawekezaji wa ndani wanaojihusisha na uandaaji pamoja na usambazaji wa maji ya kunywa ya Kitulo na kuwahimiza kukuza uwekezaji wao kwa kuwa serikali imefungua milango kwa wawekezaji kunufaika na vivutio vya uwekezaji vinavyotolewa na TIC.
