Latest Posts

FURSA LUKUKI ZABAINISHWA UWEKEZAJI WA KIWANDA CHA PAMBA KIGOMA

Mkoa wa Kigoma umetajwa kuwa miongoni mwa mikoa ya kimkakati nchini Tanzania, ukiwa na nafasi muhimu katika masoko, kilimo, na kukuza maendeleo ya kiuchumi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Gilead Teri ambaye amesisitiza umuhimu wa mkoa huo katika nyanja zote tatu na kueleza jinsi uwekezaji wa kimkakati unavyochangia maendeleo ya wakulima na jamii kwa ujumla.

Amesema kuwa mkoa wa Kigoma umejipatia nafasi maalumu katika soko la Afrika Mashariki hasa kwa nchi jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, na Uganda, na kufanya kuwa rahisi kwa bidhaa zinazozalishwa Kigoma kuuzwa katika masoko hayo na hivyo kuongeza nafasi za biashara kwa wakulima na wafanyabiashara wa mkoa.

Aidha Teri amesema kuwa uwekezaji katika miundombinu na maendeleo ya bandari umeongeza uwezo wa mkoa huo kuuza bidhaa zake kwa urahisi, hali inayoimarisha uchumi wa mkoa kwa jumla.

Ameeleza namna gani mkoa wa Kigoma unavyopata manufaa kupitia miradi ya kiuchumi akitolea mfano uwekezaji wa Shilingi bilioni 9.4 unaotarajiwa kuanza Septemba 2024 unaohusisha ujenzi wa kiwanda cha pamba kinachomilikiwa na Mtanzania kikijulikana kwa jina la NGS Investment Company Ltd, Uvinza Ginnery ambacho mpaka sasa kimekamilika kwa asilimia 98.

Amesema mradi huo utaleta mapinduzi makubwa kwa wakulima wa pamba katika mikoa ya Kigoma, Katavi, na Bariadi utakapokamilika, huku ukitarajiwa kuanza uzalishaji rasmi mwezi Septemba 2024.

Akizungumzia mradi huo wa kiwanda cha pamba, Meneja Mradi mhandisi Dions Masanja amesema uwekezaji huu unatoa fursa muhimu kwa wakulima wa pamba hasa kutoka maeneo ya Kasulu, Kakonko, na Kibondo ambao wamehamasika kulima zao hilo baada kuanzishwa kiwanda.

Aidha amesema kuwa mradi huo utakuwa chachu ya kuboreshwa kwa hali ya maisha ya wakazi wa Kigoma kwani utawawezesha wakulima kuuza mazao yao kwa urahisi hivyo kuongeza mapato yao, na kutoa ajira zaidi ya 500.

Kwa upande wake Meneja Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani kutoka TIC Felix John Meneja amesema kuwa TIC iko kwenye kampeni maalumu ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani, ambapo Kigoma ni sehemu muhimu ya mpango huo miongoni mwa mikoa mingine, lengo likiwa kuleta mabadiliko chanya katika uchumi wa mikoa hiyo.

 

Amesema uwekezaji wa karibuni una lengo la kukuza maendeleo ya viwanda, kuongeza ajira, na kuboresha huduma za jamii, hali inayoonesha jinsi Kigoma ilivyo na umuhimu mkubwa katika maendeleo ya taifa kwa jumla.

Ameongeza kuwa mchango wa mkoa wa Kigoma katika sekta za masoko na kilimo ni mkubwa, na miradi ya uwekezaji kama ile ya kiwanda cha pamba inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha hali ya maisha ya wakazi wa mkoa huo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!