“Ninawashauri wanaolima bangi waache hii tabia walime mazao mengine ili tufaidike wote kwa sababu kuna kunde, mahindi, choroko, maharage na mbaazi yote haya yanakubali. Hili eneo ni kubwa sana linaweza likatulisha sisi kijiji na kuifanya njaa isiwe gumzo. kwani kuna muda unafikaga vyakula hakuna zipo bangi tu, sisi hatuwezi kula bangi”, hii ni kauli ya Saidi Mijinga mkazi wa Kisaki mkoani Morogoro.
Yeye ni miongoni mwa vijana waliojitolea kushirikiana na Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kuteketeza mashamba ya bangi mkoani humo katika operesheni maalumu mkoani ya siku tisa katika vijiji vya Nyarutanga, Lujenge na Mafumbo vilivyopo wilaya za Morogoro vijijini na Kilosa ambapo katika vijiji vya mafumbo na Lujenge kumeteketeza jumla ya ekari 1,165 za mashamba ya bangi na kukamata kilogramu 102 za mbegu za bangi.

Akizungumza mara baada ya utekelezaji wa mashamba hayo, Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo amesema mashamba ya bangi yaliyoteketezwa yamelimwa pembezoni mwa mto Mbakana, Misigiri na Mgeta kwenye eneo la akiba la hifadhi ya Taifa Mikumi na kusababisha uharibifu mkuwa wa mazingira.
“Uharibifu mkubwa sana wa mazingira umefanyika katika eneo hili ambapo miti imekatwa ili kupata eneo la kulima bangi na hivyo kuharibu uoto wa asili. Pia uharibifu uliofanyika katika eneo la akiba la Mikumi unaharibu ikolojia ya eneo hilo na kufanya uharibifu mkubwa wa uoto wa asili na ikizingatiwa mito hiyo inatiririsha maji katika bwawa la Mwalimu Nyerere linalotegemewa kwa uzalishaji wa umeme”, amesema Lyimo.

Kadhalika, amewashukuru sana wananchi hususan vijana waliojitolea kushiriki katika zoezi zima la utekelezaji wa mashamba ya bangi pamoja na Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha mamlaka kuweza kufanya operesheni za kuteketeza mashamba ya bangi na kutokomeza dawa za kulevya nchini Tanzania.
Naye Joseph Juma Kibaya mkazi wa Nyarutanga amewaomba wananchi waendelee kuwafichua wauzaji na wafanyabiasha wa bangi kwani ina madhara makubwa kwa vijana na jamii kwa ujumla, na kuomba raia waungane na kuwa kitu kimoja kupinga bangi ili kuepuka athari zake kwa vijana na vizazi vijavyo.
Aidha, katika operesheni iliyofanyika kijiji cha Nyarutanga watu 6 wakiwa na kilogramu 342 za bangi wamekamatwa na watafikishwa mahakamani taratibu za kisheria zitakapokamilika.
