Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kupanua uwekezaji nje ya mipaka ya nchi, kama ilivyojadiliwa katika kikao kazi cha siku tatu kilichohitimishwa Ijumaa Agosti 30, 2024 jijini Arusha.
Kikao hicho, kilichofunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kilikusanya wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma kujadili mikakati ya mageuzi na uwekezaji wenye tija.

Kauli mbiu ya kikao hicho, “Mikakati ya Taasisi na Mashirika ya Umma Nje ya Tanzania,” ililenga namna taasisi na mashirika ya umma yanavyoweza kupanua wigo wao nje ya soko la ndani, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais aliyoyatoa mwaka jana ya kutafuta fursa za kimataifa.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Adam Mihayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, alisisitiza umuhimu wa kufanya tafiti za kina ili kuelewa masoko lengwa kabla ya kupeleka huduma nje ya mipaka ya Tanzania.
“Ili kufanikiwa nje ya mipaka ya Tanzania, ni lazima tulitambue soko lengwa kwa kufanya tafiti za kina ili kubaini mianya ya fursa na kutengeneza bidhaa na huduma zetu kadri ya mahitaji ya soko la kimataifa,” alisema Mihayo.
Mihayo alieleza pia umuhimu wa kuunda ubia wa kimkakati na kushirikiana na mashirika mengine ili kutumia mtandao wa ndani na utaalamu wao.
“Muundo wetu wa kibiashara unatakiwa uwe wa kibunifu na wenye uwezo wa kubadilika kuendana na mazingira, ili kukabiliana na mahitaji tofauti tofauti ambayo ni muhimu ili kufanikiwa katika soko la kimataifa.”
Kwa upande wa ushirikiano baina ya taasisi za umma, Mihayo alisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja kwa kushirikishana takwimu, kupanga mikakati kwa pamoja, na kusaidiana katika utoaji wa huduma.
“Kwa kufanya hivyo, tutaboresha rasilimali zetu na pia tutawapa wateja wetu huduma bora kulingana na mahitaji yao na kujenga imani yao kwetu,” alisema.
Akizungumzia mafanikio ya hivi karibuni, Mihayo alielezea jinsi TCB ilivyozindua huduma za kibenki kwa Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora Banking) nchini Comoro.
“Hii inaonesha dhamira yetu ya kutoa huduma za kibenki nje ya mipaka na kuyafikia mahitaji ya Watanzania wote dunia nzima,” alisema Mihayo, na kuongeza kuwa TCB inatarajia kuingia katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ndani ya miaka miwili ijayo, hivyo kumpa kila Mtanzania fursa ya kumiliki hisa na kuwa sehemu ya mafanikio ya taasisi hiyo.
Mihayo alihitimisha kwa kutoa wito kwa taasisi na mashirika ya umma kuiga mfano wa mataifa mengine yaliyofanikiwa kupenyeza biashara zao nchini Tanzania.
“Wametuonesha kwamba inawezekana kufanya hivyo, ni wakati wetu sasa kuthubutu na kutumia fursa hii. Tushirikiane, tuwe wabunifu, na kupanga mikakati ili kuhakikisha kwamba taasisi na mashirika ya umma yanajitegemea, yanachangia pato la taifa, na kuwa miongoni mwa mashirika makubwa duniani.”, alisema Mihayo.