Latest Posts

JAMII YAKUMBUSHWA KUSAIDIA WENYE UHITAJI

Na Linda Akyoo, Kilimanjaro.

Jamii imetakiwa kuwa na utamaduni wa kusaidia watu wenye uhitaji hasa makundi maalumu yenye mahitaji ya kipekee, na kutenda matendo ya huruma.

Wito huu umetolewa na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Kusaidia Jamii Tanzania (TACOSO) Stanley Urassa wakati wa kukabidhi vifaa mbalimbali kwa kituo cha Watoto Yatima Kilimanjaro (COKO) kilichopo Soweto mkoani Kilimanjaro.

Urassa ameikumbusha jamii kuwa suala la kutembelea na kuwafariji wahitaji si jukumu la Taasisi au Serikali pekee, bali ni la kila mtu na jamii kwa ujumla.

Aidha Urassa amesema kuwa huduma zitolewazo kwa wahitaji ziende kwenye makundi ya wahitaji ikiwamo wazee, wajane na watoto na kuiomba serikali itenge fungu la watu wenye uhitaji.

Naye Mjumbe wa bodi ya Shirika hilo, Bi. Witness Urio amesisitiza kuwa TACOSO imejizatiti kuwahudumia wahitaji ikiwa ni pamoja na watoto yatima, wazee, wenye changamoto za ulemavu, na wagonjwa.

“Jukumu la jamii ni kurudisha kidogo kwa wahitaji ambao ni sehemu ya jamii tunayoishi. Kugusa mahitaji yao ya msingi na kutenda matendo ya huruma kwao ni muhimu sana,” amesema Bi. Urio.

Kwa upande wake msimamizi wa kituo hicho, Bi. Fatma Hussein ametoa shukrani za dhati kwa uongozi wa TACOSO na kusema misaada hiyo imekuwa faraja kubwa na imeweza kurudisha tabasamu kwa watoto wenye uhitaji. Ameomba taasisi nyingine kuendelea kusaidia kituo hicho kwa hali na mali.

Shirika la TACOSO, lililoanzishwa mwaka 2020, linajitahidi kusaidia jamii kupitia matendo ya huruma na linatekeleza shughuli zake katika mikoa ya kaskazini. Hadi sasa shirika hilo limeweza kufikia vituo vya wahitaji zaidi ya 13 kwa misaada ya kibinadamu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!