Kampuni ya Peachy Village Company Limited imeifungulia kesi Benki ya CRDB (CRDB Bank PLC) kwa kitendo kinachodaiwa kuwa cha kufungua akaunti ya benki kwa jina la kampuni hiyo bila ridhaa au idhini ya wamiliki wake. Akaunti hiyo yenye namba 015c763701500 ilifunguliwa kinyume na taratibu, na imedaiwa kwamba benki hiyo iliruhusu watu wasiojulikana kujipatia fedha isivyo halali kiasi cha shilingi 13,213,200/= ambazo Peachy Village Company Limited ilipaswa kulipwa kutokana na huduma ilizotoa katika kituo cha afya cha Rudi kilichopo Mpwapwa.
Kesi hiyo ya madai, yenye shauri namba 14845 ya mwaka 2024, imefunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma na kwa sasa iko kwenye hatua ya upatanishi wa mahakama (Court annexed Mediation). Tarehe 02 Septemba 2024, wadaiwa wote walikutana na mpatanishi aliyechaguliwa na mahakama kwa ajili ya upatanishi, lakini juhudi za upatanishi ziligonga mwamba na hivyo faili litarudishwa kwa hakimu anayesikiliza kesi hiyo kwa ajili ya kutoa maelekezo zaidi na kuendelea na usikilizaji wa shauri hilo.
Wakili wa mlalamikaji, Chacha Zakayo Mwita, alipoulizwa na mwandishi wa habari wa Jambo TV kuhusu shauri hilo, alithibitisha kuwa mteja wake, Peachy Village Company Limited, amefungua shauri hilo dhidi ya CRDB Bank kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni uzembe na nia ovu ya benki kufungua akaunti ya benki kwa jina la kampuni hiyo bila ridhaa au idhini ya wamiliki wake.
“Kitendo cha mdaiwa kufungua akaunti kwa jina la mteja wangu bila ridhaa ni kitendo cha kizembe na chenye nia ovu, ambacho kimesababisha watu wasiojulikana kujipatia isivyo halali fedha za mteja wangu kiasi cha shilingi 13,213,200/=. Hii ndiyo sababu mteja wangu ameamua kufungua shauri hili mahakamani ili kutafuta haki yake”, alisema wakili huyo.
Katika shauri hilo, mlalamikaji ameomba mahakama itoe amri kwa CRDB Bank kutamka kwamba walifungua akaunti hiyo kinyume cha sheria na kwa uzembe mkubwa, jambo ambalo liliwawezesha watu wasiojulikana kujipatia kiasi hicho cha shilingi 13,213,200/= bila idhini wala ridhaa ya Peachy Village Company Limited. Aidha, mlalamikaji ameomba mahakama iamuru benki hiyo kuilipa kampuni hiyo kiasi hicho cha fedha ambazo inadaiwa kuwa waliwasaidia watu wasiojulikana kuzichukua isivyo halali kupitia akaunti iliyofunguliwa.
Pia, mlalamikaji ameomba fidia ya ziada ya shilingi 107,112,125/= (Million mia moja na saba laki moja na elfu kumi na mbili na mia moja ishirini na tano) kama fidia ya hasara mbalimbali ambazo kampuni hiyo imepata kutokana na akaunti hiyo kufunguliwa bila idhini yao.
Wakili wa mlalamikaji ameeleza kuwa Peachy Village Company Limited imepata hasara kubwa ya kifedha kutokana na kitendo hicho, ikiwa ni pamoja na kushindwa kuendesha biashara zake, kushindwa kutoa huduma kwa wateja wake, na kushindwa kulipa madeni.
Wakili huyo alisema kuwa hasara hiyo ilianza kutokea tarehe 19 Oktoba 2023, siku ambayo mlalamikaji alitoa taarifa rasmi kwa benki kuhusu akaunti hiyo iliyofunguliwa isivyo halali.
Mbali na fidia ya hasara ya moja kwa moja, mlalamikaji pia ameomba fidia ya Shilingi milioni 500 kwa hasara zisizo za kifedha ambazo kampuni hiyo imepata. Miongoni mwa hasara hizo ni pamoja na kuathirika kwa sifa na picha au chapa ya kibiashara ya Peachy Village, msongo wa mawazo uliosababishwa na hali hiyo, pamoja na kuharibika kwa uhusiano wa kibiashara wa kampuni hiyo na washirika wake.
Kwa upande wake, Benki ya CRDB kupitia kwa wakili wake wa utetezi, Teckla Kimati, amethibitisha kuwa kesi hiyo ipo mahakamani lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu utetezi wao.