Latest Posts

MBUNGE LONGIDO ASHUKURU ALIYEKUWA DC LONGIDO KUTENGULIWA

Mbunge wa jimbo la Longido mkoani Arusha ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Lemomo Kiruswa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uamuzi wake wa kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido, Marko Ng’umbi.
 
Akizungumza katika Mkutano wa hadhara katika Kata ya Mundarara, Dkt. Kiruswa amesema uamuzi huo umeirudisha heshima katika wilaya ya Longido, akieleza kuwa uongozi wa awali ulikuwa na changamoto kutokana na kauli na vitendo vya Ng’umbi, ambavyo vilidhalilisha viongozi wa wilaya, wakiwemo viongozi wa mila na watumishi wa Halmashauri. Aliongeza kuwa viongozi hao walimvumilia kwa muda kutokana na hekima na ustaarabu wa jamii ya kimaasai, inayothamini amani na nidhamu.
 
“Hata hivyo, baada ya kauli zake za kudai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliiba uchaguzi wa 2020, tuliona kuwa imefika wakati wa mabadiliko. Wilaya ya Longido ni ngome ya CCM, na watu wake wanashinda kwa haki kupitia uchaguzi huru na wa wazi tangu enzi za mzee Lekule,” aliongeza Dkt. Kiruswa.
 
Kwa upande wake, Mkuu mpya wa Wilaya ya Longido, Salum Kali, aliahidi kuwatumikia wananchi kwa uadilifu, akieleza kuwa atapatikana kwa wananchi saa 24 kwa namba ya simu atakayowagawia. Pia aliahidi kushughulikia kero zao, ikiwemo suala la daraja na upatikanaji wa zahanati.
 
“Nitapita kijiji kwa kijiji kuhakikisha serikali inatatua kero zenu, hususan shida ya malisho, kwani mimi ni mwakilishi wa Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Salum Kali.
 
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Amos Makalla, aliwaomba radhi wananchi wa Longido kwa matamshi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya, akisema yalilenga kuwachonganisha na hayawakilishi msimamo wa CCM. Aliongeza kuwa CCM inajivunia kushinda kihalali na inafuata misingi ya uchaguzi huru.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!