Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, ametangaza tukio la kutekwa kwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Taifa ya chama hicho, Ally Mohamed Kibao.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Ijumaa, Septemba 6, 2024, eneo la Kibo, karibu na Tegeta, wakati Kibao akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Tanga kwa basi la Tashrif.
Mnyika akizungumza na wanahabari mchana wa siku ya Jumamosi Septemba 7, 2024 Makao Makuu ya CHADEMA, Dar es Salaam ameeleza kuwa basi hilo lilizuiwa na magari mawili ambayo hayakuwa na nembo yoyote na watu waliokuwa ndani ya magari hayo walikuwa na silaha.
“Walikwenda moja kwa moja kwenye kiti alichokaa Mzee Ally Mohamed Kibao, wakamchukua kwa nguvu na hata kumshambulia kabla ya kuondoka naye,” alisema Mnyika, akiongeza kuwa watu hao hawakujitambulisha kama polisi, jambo ambalo linatia shaka kuhusu uhalali wa tukio hilo.
Katibu Mkuu huyo wa CHADEMA amedai kuwa bunduki walizotumia waliomchukua Kibao ni aina zinazotumiwa zaidi na Idara ya Usalama wa Taifa kuliko Jeshi la Polisi, akitoa wito kwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa kujitokeza na kueleza kama idara hiyo inahusika na tukio hilo.
“Kwa kawaida huwa tunajizuia sana kuzungumza kuhusu Idara ya Usalama wa Taifa lakini kwa sheria ya idara ya Usalama wa taifa kuna mtu mmoja tunaweza tukamtaja na tunaweza kumzungumza, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa natoa wito kwake ajitokeze aeleze iwapo idara ya usalama wa taifa imemteka Mzee Ally Mohammed Kibao, yuko wapi?”, ameeleza Mnyika.
Aidha, Mnyika alikumbusha umuhimu wa waangalizi wa uchaguzi kufuatilia mwenendo wa uchaguzi nchini, akitoa wito kwa taasisi za ndani na nje kuomba nafasi za kuwa waangalizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa kabla ya tarehe 17 Septemba 2024.
“Nitoe wito kwa taasisi za ndani na nje kuomba nafasi ya kuwa waangalizi wa uchaguzi kwa muda uliobaki,” alisema Mnyika, akieleza umuhimu wa taasisi hizo kufuatilia uchaguzi katika kila eneo nchini ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi na haki.