Latest Posts

CHAMA CHA CUF CHALAANI MAUAJI YA MJUMBE WA CHADEMA, MZEE ALI KIBAO

Chama cha Wananchi (CUF) kimeelezea masikitiko yake makubwa na kulaani vikali mauaji ya Ali Mohamed Kibao, mjumbe wa Sekretarieti Kuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
 
Marehemu Kibao aliripotiwa kushushwa kwenye basi eneo la Tegeta na watu wanaodaiwa kuwa askari kabla ya mwili wake kupatikana akiwa tayari ameuawa.
 
Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa CUF, Eng. Mohamed Ngulangwa, chama hicho kimesema kimepokea kwa mshtuko mkubwa matukio yanayoendelea nchini ya kupotea kwa watu, na mwishowe kugunduliwa wakiwa wameuawa.
 
Amesema mauaji hayo yameanza kuleta hofu kwa wananchi, hasa kutokana na baadhi ya viongozi wa CCM kushuhudiwa wakitoa matamshi kwamba jeshi la Polisi halipaswi kushughulika na watu wanaopotea.
 
“Hali hii inatengeneza taharuki kwa wananchi na kuathiri juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kurejesha hali ya amani na kuaminiana miongoni mwa Watanzania,” ilisema sehemu ya taarifa ya CUF.
 
CUF imetoa wito kwa vyombo vya dola kuhakikisha wahusika wa ‘unyama’ huo wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria mara moja. Chama hicho pia kimetoa pole kwa familia ya marehemu Kibao, CHADEMA, na wote walioathirika na msiba huo.
 
“Hakika sote ni wa Allah na kwake tutarejea,” alimalizia Eng. Ngulangwa, akimwombea marehemu apumzike kwa amani huku akiomba Mwenyezi Mungu awape wafiwa subira.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!