Kutokana na ongezeko la wasiwasi kuhusu watoto kupotea katika mazingira ya kutatanisha, wananchi wa Kijiji na Kata ya Bulela, Wilaya ya Geita, wamekutana kujadili namna ya kuimarisha ulinzi wa watoto wao.
Mikakati iliyowekwa inajumuisha kuwataka walimu kuwatoa watoto mapema shuleni na kuzuia watoto kwenda maeneo ya ‘senta’ nyakati za usiku.
Diwani wa Kata ya Bulela, Salome Ndekeja, ametoa wito huo wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara, akisisitiza umuhimu wa kila mmoja kuchukua jukumu la kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya utekaji ambavyo vimeongezeka katika maeneo mbalimbali.

“Ni muhimu sana kama jamii kuhakikisha tunachukua hatua za haraka kuwalinda watoto wetu. Hali ya sasa inaogopesha, na kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha watoto wanarudi nyumbani mapema na hawashiriki shughuli za usiku kwenye senta,” alisema Salome.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Bulela wamesema wameamua kuchukua hatua za tahadhari kwa kuweka ulinzi wa kijiji kutokana na hofu kubwa juu ya usalama wa watoto wao.
“Tumekuwa na wasiwasi mkubwa. Sasa hivi tunapanga doria za pamoja ili kuhakikisha watoto wetu wanakuwa salama muda wote,” amesema Ernest Shululu.
“Tunawaomba wazazi wenzetu wasiruhusu watoto wao kwenda senta au maeneo ya mbali nyakati za usiku. Tumeona hatari kubwa,” amesema Agnes Shiluka, mkazi wa Kijiji cha Bulela.

Hatua hizi zinatarajiwa kuleta faraja kwa wazazi wa Kijiji cha Bulela, huku viongozi wakisisitiza ushirikiano wa karibu kati ya walimu, wazazi, na viongozi wa kijiji ili kufanikisha mpango wa ulinzi wa watoto.