Latest Posts

UJENZI WA BANDARI MPYA YA MBAMBA BAY KULETA AJIRA

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari hapa Tanzania (TPA) imesema kuwa ujenzi wa bandari mpya ya kisasa ya Mbamba Bay, unaogharimu bilioni 75.8, ni mradi wa kimkakati utakaonufaisha taifa kwa njia nyingi, siyo tu wakati wa ujenzi, bali hata baada ya kukamilika.

Akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ya kukagua eneo la mradi katika wilaya ya Nyasa, Naibu Mkurugenzi wa TPA, Juma Kijavara, amesema faida kubwa ya mradi ni upatikanaji wa ajira kwa wananchi, hususan vijana, hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika familia na wilaya hiyo kwa ujumla.

Kijavara ameongeza kuwa fursa za biashara zitapanuka kupitia huduma kwa mkandarasi na wafanyakazi wa mradi.

 

“Hii itaongeza kipato kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati wakati wa utekelezaji wa mradi wa miaka miwili,” alisema.

Aidha amesema kuwa ujenzi wa miundombinu kama vile barabara, maji, na umeme ni faida nyingine kwa wananchi wa eneo hilo.

Ameongeza kuwa bandari hiyo itakuza uchumi wa Tanzania na nchi jirani za Malawi, Msumbiji, na Zambia, na kuhamasisha uwekezaji zaidi katika sekta binafsi na umma, hususan katika viwanda, usafirishaji, biashara, na utalii wa Ziwa Nyasa.

Waziri Mbarawa alisifu TPA kwa utekelezaji wa mradi huu na utendaji kazi mzuri wenye tija kwa taifa

“Bandari hii ya kisasa itapunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa za viwandani, hususan madini, mazao ya kilimo na uvuvi, kwa uwezo wake wa kupokea meli kubwa, hivyo kupunguza gharama na kuleta unafuu wa bei kwa wananchi.” Amesema Mbarawa.

Aidha, ametaja mradi mwingine wa matanki ya kuhifadhi mafuta kwenye bandari ya Dar es Salaam, akisisitiza juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza uchumi na kufungua fursa za biashara.

Ujenzi wa bandari hii unahusisha ujenzi wa gati mbili zenye urefu wa mita 103, maghala, nyumba za watumishi, jengo la utawala, na maeneo mengine muhimu, ikiwa ni pamoja na barabara za ndani na nje.

Mhandisi wa mradi huo kutoka TPA, John Paul, alithibitisha kuwa mkandarasi ameshapata malipo ya awali ya shilingi 3,261,529,017.63, sawa na asilimia 5, na malipo kwa Mhandisi Mshauri ya shilingi 448,192,240.70, sawa na asilimia 10.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!