Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongeza mchango mkubwa wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) katika kuboresha miundombinu ya barabara na reli nchini.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, Jumatano, tarehe 25 Septemba 2024, Rais Samia alizindua barabara ya Mbinga – Mbambabay yenye urefu wa kilomita 66 na kueleza namna uwekezaji huo unavyorahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa.

Katika hotuba yake, Rais Samia amesisitiza kuwa AfDB imekuwa mshirika mkubwa katika sekta ya miundombinu nchini, akitaja mchango wa benki hiyo sio tu katika ujenzi wa barabara hii, bali pia katika miradi mingine ya kitaifa.
“AfDB hawajasaidia barabara hii pekee, ni wadau wetu wa barabara nchi nzima, na hivi tunavyozungumza wanatusaidia sana kujenga barabara za mzunguko pale katika mji mkuu Dodoma, barabara nne kwa nne kila upande,” amesema Rais.
Rais Samia pia amefichua kwamba Benki ya Maendeleo Afrika kwa mara ya kwanza imehusika katika kusaidia ujenzi wa reli ya SGR eneo la Kigoma, ikihusisha pia kuunganisha reli hiyo na nchi ya Burundi. Ametoa shukrani kwa AfDB kwa ushirikiano wao katika miradi mikubwa ya kitaifa inayolenga kuinua uchumi na kuboresha usafiri.

Akizungumzia umuhimu wa barabara mpya ya Mbinga – Mbambabay, Rais Samia amesema uwepo wake utarahisisha safari na biashara kwa wakazi wa Nyasa na maeneo ya jirani. Amekumbusha hali ngumu ya usafiri kabla ya ujenzi wa barabara hiyo, akiwataka wananchi kutumia miundombinu hiyo mpya kwa maendeleo yao na kuhimiza tahadhari kwa madereva ili kuepusha ajali.
“Uwepo wa barabara hii umeleta faraja kubwa kwamba unakwenda kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa… Niwaombe ndugu zangu kuitumia barabara hii kuleta maendeleo ndani ya wilaya yetu,” amesema Rais, akisisitiza umuhimu wa kuwa waangalifu barabarani ili kuzuia ajali.
