Latest Posts

RAIS SAMIA: SERIKALI ITAENDELEA KUINUA KILIMO KWA RUZUKU NA HUDUMA ZA UGANI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaahidi wananchi wa Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma kuwa serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya kilimo kutokana na umuhimu wake mkubwa kwa uchumi wa taifa.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Litola tarehe 26 Septemba 2024, Rais Samia amesema kilimo kimeibuka kama sekta muhimu inayochangia pato la taifa kwa haraka na kuwahakikishia wananchi kuwa serikali itaendelea kuwekeza zaidi kwenye sekta hiyo.
“Serikali itaendelea kuwa nanyi kwenye sekta ya kilimo,” amesema Rais Samia, akifafanua kuwa sekta hiyo imethibitisha uwezo wake wa kuzalisha kwa haraka na kutoa mapato kwa taifa.
Amewaeleza wananchi kuwa serikali imeweka ruzuku ya mbolea na imepanga pia kuweka ruzuku ya mbegu. Aidha, Rais Samia ameagiza miche ya kahawa, mazao muhimu katika mkoa wa Ruvuma, itolewe bure kwa wakulima, huku jitihada zikiongezwa kwenye huduma za ugani ili kuboresha uzalishaji.
Rais Samia amewasihi wananchi waendelee kufanya kazi kwa bidii ili kukuza kilimo na kuchangia katika uboreshaji wa sekta nyingine kama elimu, afya, na miundombinu ya barabara.
“Tukuze kilimo, tukuze afya zetu, tujenge shule kwa ajili ya watoto wetu, tujenge barabara tusafirishe mazao yetu sisi wenyewe,” amesema Rais, akisisitiza kuwa serikali ina malengo makubwa ya kuendeleza kilimo ili kiwe chanzo kikubwa cha mapato kwa taifa.
Akizungumza kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 2024, Rais Samia amehimiza wananchi wote kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la kuchagua wenyeviti wa vitongoji, vijiji, na kamati zao.
Amewataka wale wenye sifa za kugombea wajitokeze kwa uhuru bila mizengwe, huku akiwahimiza wananchi kutokwenda kinyume na haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka.
“Wale wenye sifa za kuchagua ninaomba wananchi wote twendeni tukachague. Haijuzu wewe unategea kwenda kuchagua, wengine wanakwenda kuchagua unakaa kwenye vikao huko unaanza kulalamika,” amesema Rais Samia, akisisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza na kuchagua viongozi bora watakaosaidia kusimamia maendeleo ya maeneo yao.
Amewahimiza wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo kwenye sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, maji, umeme, na kilimo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!