Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere imeingia makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Renmin nchini China kwa mara ya pili, ikiwa na lengo la kuboresha mafunzo, utafiti, na kubadilishana wataalamu.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Mkuu wa shule hiyo, Profesa Marcellina Chijoriga, na kiongozi wa Chama Tawala cha China (CPC) kwenye chuo hicho, Zhang Donggang, katika hafla iliyohudhuriwa na wakufunzi wa vyuo mbalimbali nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Chijoriga amesema, “Makubaliano haya yatakuwa ni kwa ajili ya kubadilishana wataalamu, ambapo wataalamu wetu watakuja China na wale wa China watakuja Tanzania. Hii ni sehemu ya kubadilishana uzoefu.” Ameongeza kuwa, “Chuo hicho ni kikubwa sana na kimejikita katika masuala ya utafiti wa uandishi wa vitabu, na ushirikiano huu utakuwa na manufaa makubwa kwa pande zote mbili.”
Profesa Chijoriga amesisitiza umuhimu wa Chuo cha Renmin katika kutoa mafunzo kwa viongozi wa chama na serikali, akisema, “Faida hii ni kwa vyama sita vya ukombozi Kusini mwa Afrika, ambapo China imekuwa msaidizi mzuri.” Alitaja vyama vya ukombozi kama vile CCM, FRELIMO, SWAPO, ANC, na ZANU-PF.
Aidha, Dk. Evaristo Haule, Naibu Mkuu wa Chuo, ameeleza kuwa, “China imefanikiwa, na tumeona namna wanavyofanya kazi kwa bidii. Tunapaswa kujifunza kutoka kwao.” Ameongeza kuwa, “Kwa kupitia mkataba huu, tutajenga uwezo wa viongozi wa chama na serikali.”
Kwa upande wake Dkt. Theresia Dominic kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesisitiza umuhimu wa nidhamu ya kazi na fedha, akisema, “Mchina ana nidhamu ya juu katika utendaji wake wa kazi. Watanzania tunapaswa kujifunza tabia hizi ili kuboresha maisha yetu.” Ameongeza kuwa, “Wachina wanatilia maanani afya zao, na tunapaswa kuiga tabia hiyo.”
Kiongozi wa CPC, Zhang Donggang, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya nchi za Afrika na China, akisema, “Tunahitaji kushirikiana ili kupiga hatua katika masuala ya kimaendeleo. Umoja wetu umekuwa na mafanikio makubwa.”
Ushirikiano huu unatarajiwa kuimarisha uhusiano wa kitaaluma kati ya nchi hizi mbili, huku ukitoa fursa za kuboresha elimu na mafunzo kwa viongozi wa kisasa.