Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA (BAWACHA), Catherine Ruge, ametoa pongezi kwa Tundu Lissu kufuatia ushindi wake wa nafasi ya uenyekiti wa CHADEMA taifa katika uchaguzi wa ndani ya chama hicho.
Kupitia chapisho la siku ya Alhamisi Januari 23, 2025 la ukurasa wake wa X, Ruge amempongeza Lissu kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Pia amemshukuru Freeman Mbowe, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, kwa mchango wake mkubwa katika kujenga chama na kuimarisha demokrasia ndani ya CHADEMA.
“Hongera sana Mhe. Tundu Lissu kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti Mpya wa Chama chetu kwa miaka mitano ijayo, nakutakia kheri katika kutekeleza majukumu yako mapya.” Amesema Ruge.

Katika ujumbe wake, Ruge ametoa shukrani maalum kwa Freeman Mbowe kwa miaka yake 21 ya uongozi wa CHADEMA, akimtaja kama kiongozi aliyejenga misingi imara ya chama hicho. Aidha, alimtakia kila la heri Mbowe katika maisha yake mapya nje ya nafasi ya uongozi wa moja kwa moja.
“Freeman Mbowe, asante kwa kutujengea chama kwa ukubwa huu, asante kwa utumishi wako wa miaka 21. Nakutakia kheri katika maisha yako mapya. Nawashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kuonesha kuwa Chadema tunaiishi Demokrasia kama lilivyo jina la chama chetu.” Ameandika Ruge katika chapisho lake.