Serikali imelalamikiwa kutoweka wazi mchakato mzima wa bajeti hasa kwa wananchi waishio vijijini na badala yake wanashuhudia miradi ya maendeleo ikiendelea kutekelezwa bila ushirikishwaji.
Kauli hizo zimetolewa Jumamosi Machi 15, 2025 Jijini Dodoma na wakulima wa wilaya za Chamwino (Dodoma) na Halmashauri ya Singida walioshiriki mafunzo ya kuwajengea uwezo ambayo yameandaliwa na Shirika la Action Aid kupitia mradi wa Trasnformative Impact Fund (TIF) ili kuwapa mbinu za kuhoji miradi na mwanzo wa bajeti.
Akizungumza kuhusu mpango huo, mkulima Sendeu Mjelwa kutoka kijiji cha Msanga wilaya ya Chamwino amesema hakuna bajeti shirikishi zinazoanzia ngazi ya chini vijijini badala yake yanapelekwa maagizo kutoka ngazi ya juu na ndiyo maana utekelezaji wake umekuwa na changamoto hasa miradi mikubwa inayojengwa.

Sendeu amesema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi wa vijijini hasa wakulima wakihoji namna gani wanashushiwa bajeti kutoka mamlaka za juu bila ya kujua nani aliamua kujenga mradi au kutoa kiasi cha fedha kwa ajili ya kitu chochote kwenye kijiji.
Hata hivyo ofisa Kilimo na Mifugo kutoka Halmashauri ya Singida Adam Sungita amesema ushiriki wa wananchi katika bajeti ni mkubwa na mara nyingi huanzia ngazi ya chini kwa wananchi wenyewe.
Sungita amesema ushiriki wa kuandaa bajeti siyo lazima ujikite kwenye pesa bali wananchi wanaweza kukaa na kuibua mradi au shughuli nyingine.
Ofisa huyo amesema mara nyingi watu wanalalamika mapato ya vijiji vyao hayajulikana kwenye matumizi kwa madai yanachukuliwa na Halmashauri, lakini wanasahau kuwa kijiji Fulani kinaweza kuwa na uwezo wa kukusanya Shilingi milioni 14 wakati kijiji kingine kikakusanya hadi Shiligi milioni 200, na pesa hizo hupaswa kuwekwa katika mfuko mmoja, kisha zifanyiwe mgao katika maendeleo.