Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala, iliyopo Kibaha Vijijini, mkoani Pwani, ni hatua muhimu katika kupunguza msongamano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza ufanisi wa huduma za usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili Machi 16, 2025 katika eneo la Bandari Kavu ya Kwala, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kuwa bandari hiyo imejengwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa gharama ya shilingi bilioni 83, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuboresha mfumo wa usafirishaji wa mizigo.
“Tumeamua kujenga bandari hii hapa Kwala ili kupunguza msongamano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, kwani awali kulikuwa na bandari kavu ndogo ndogo (ICDs) 11 zilizoshindwa kuhimili wingi wa makontena,” amesema Msigwa.

Bandari ya Kwala inapatikana umbali wa kilomita 90 kutoka Bandari ya Dar es Salaam na kilomita 15.5 kutoka barabara kuu, jambo linaloifanya kuwa eneo muhimu la kuhifadhi mizigo.
“Eneo hili limeandaliwa kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya kupokelea na kuhifadhi mizigo kwa usalama. Makontena yaliyohifadhiwa hapa hayachafuki na yako salama kwa kiwango cha juu,” ameongeza Msigwa.
Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo, serikali imesafisha eneo kubwa, kujenga yadi kubwa ya kuhifadhi makontena na kuunganisha bandari hiyo na reli ya mchepuko (MGR) yenye urefu wa kilomita 1.3. Reli hiyo iliyogharimu shilingi milioni 677 imekamilika kwa asilimia 100%, na tayari inatoa huduma za kusafirisha mizigo kwa njia ya reli badala ya barabara ili kupunguza uharibifu wa miundombinu ya barabara kuu.

Kwa sasa, Bandari ya Kwala ina uwezo wa kuhifadhi makontena 300,000 kwa mwaka, ikiwa ni sawa na asilimia 30 ya makontena yote yanayoshushwa katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa siku, bandari hiyo ina uwezo wa kuhudumia makontena 823, hatua ambayo imepunguza mzigo mkubwa uliokuwa ukielekezwa moja kwa moja Dar es Salaam. Msigwa ameeleza kuwa jitihada hizi zinalenga kurahisisha upakuaji na usambazaji wa mizigo kwa wafanyabiashara ndani na nje ya nchi.
“Tunahakikisha mizigo inasafirishwa kwa ufanisi zaidi kupitia reli na barabara. Hatua hii pia itavutia wafanyabiashara kutoka nchi jirani kutumia Bandari ya Dar es Salaam badala ya bandari nyingine walizokuwa wakizitumia,” amesisitiza Msigwa.
Mbali na Kwala, serikali inatekeleza mpango wa kujenga bandari kavu katika maeneo mengine muhimu kama Dodoma, Tabora, Isaka, Mwanza, na maeneo ya mpakani karibu na Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kwa mujibu wa Msigwa, ongezeko la bandari kavu litaimarisha biashara, kupunguza muda wa usafirishaji wa mizigo na kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, ambayo tayari inaonesha dalili za kuzidiwa kutokana na ukuaji wa biashara.
“Kwa kuwepo kwa Bandari ya Kwala na bandari nyingine tunazojenga, changamoto ya msongamano wa mizigo Dar es Salaam itakuwa historia,” amesema.