Jamii ya Kimasai wilayani Monduli, mkoani Arusha, wamezindua rasmi Kituo cha Kuhifadhi Mila na Desturi za jamii yao katika kijiji cha Esilalei, kata ya Esilalei. Uzinduzi huu ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia shughuli za utalii wa kiutamaduni.
Kituo hicho kimejengwa kwa ushirikiano kati ya jamii ya kimaasai na shirika lisilo la kiserikali la ALMASI TZ, linalotekeleza shughuli zake wilayani Monduli. Lengo kuu ni kudumisha na kuenzi utamaduni wa Kimasai sambamba na kuuwezesha kuwanufaisha kiuchumi wakazi wa eneo hilo, hasa wanawake.

Akisoma risala ya uzinduzi kwa niaba ya shirika la ALMASI TZ, Mkurugenzi Mark Mamasita alieleza kuwa kituo hicho kitakuwa nguzo muhimu ya kuhifadhi, kutunza, na kuendeleza mila za jamii ya Kimasai. Aliongeza kuwa kupitia kituo hiki, wageni kutoka ndani na nje ya nchi watapata fursa ya kujifunza kuhusu maisha, mavazi, lugha, na utamaduni wa Kimasai.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Esilalei, Wilson Lengima, alieleza furaha yake kutokana na uwepo wa kituo hicho, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa kukuza utamaduni wa Kimasai na kuwapa wananchi njia mbadala ya kujipatia kipato kupitia utalii.

Wananchi wa jamii ya Kimasai nao walionesha matumaini makubwa juu ya kituo hicho, wakieleza kuwa kimekuja kwa wakati muafaka kusaidia kulinda maadili, mila na tamaduni zao, huku kikiwapa fursa za kiuchumi hasa kwa wanawake na vijana.