Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Mary Chatanda, ametoa wito mzito kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa UWT Taifa kuhakikisha wanatenda haki, kudumisha maadili ya chama na kuepuka tamaa ya fedha katika kuchagua wawakilishi wa makundi maalum ya ubunge.
Akizungumza Jumamosi, Agosti 2, 2025 jijini Dodoma, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo maalum uliowakutanisha wajumbe 986 kutoka nchi nzima, Chatanda alieleza kuwa wagombea wote waliopitishwa na Kamati Kuu ya CCM wana sifa zinazofanana, na hivyo uamuzi wa kuchagua unapaswa kuongozwa na uadilifu na si uwezo wa kifedha wa mgombea.

“Niwaombe sana wajumbe wa Mkutano Mkuu, tendeni haki, msiwachague watu kwa sababu ya fedha zao,” alisisitiza Chatanda huku akishangiliwa na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo.
Akitaja makundi yanayogombewa, Chatanda alisema ni pamoja na kundi la NGOs, wafanyakazi, wasomi wa vyuo vikuu, na watu wenye ulemavu, akieleza kuwa wote wana nafasi sawa ya kupewa dhamana ya kulisaidia taifa kupitia Bunge.
Aidha, alikumbusha wajumbe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa, na hivyo ni wajibu wa kila mwanachama wa CCM kuunga mkono juhudi hizo kwa vitendo.

“Hii vita ya rushwa ni ya kwetu sote, na haipaswi kufumbiwa macho popote pale ilipo,” alisema Chatanda.
Mkutano huu unatarajiwa kumalizika kwa uchaguzi wa wawakilishi watakaowakilisha makundi maalum katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.