Chama cha ACT Wazalendo kupitia Tawi la Mafifi, kata ya Kihesa mkoani Iringa, kimemvua rasmi uanachama Monalisa Joseph Ndala kwa madai ya kushindwa kutekeleza matakwa ya Katiba ya chama hicho, hatua ambayo inatajwa kuhusiana na mvutano wa karibuni juu ya uteuzi wa mgombea urais.
Kwa mujibu wa barua rasmi ya tarehe 28 Agosti 2025 iliyosainiwa na Katibu wa ACT wa tawi hilo, Neema Ernest Kivamba kwenda kwa Monalisa, kikao cha tathmini cha Kamati ya Uongozi ya ACT kilibaini Ndala amepoteza sifa za kuwa mwanachama hai chini ya Katiba ya chama ya mwaka 2015 (toleo la 2024).
“umepoteza sifa za kuwa Mwanachama halali na hai wa Chama cha ACT Wazalendo kwa mujibu wa Katiba ya ACT Wazalendo ya Mwaka 2015 Toleo la Mwaka 2024, Ibara ya 8 (2) (a) (b) na Ibara ya 13 (1) (c) (d) Pamoja na Ibara ya 97 (b) (d)”, imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Uamuzi huo umeambatana na kufutwa kwa kadi yake ya uanachama na kuondolewa jina lake katika regista ya wanachama wa Tawi la Mafifi.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Ndala kupinga uhalali wa mchakato wa uteuzi wa Luhaga Joelson Mpina kuwa mgombea urais wa ACT-Wazalendo, akidai ulikiuka kanuni kwa kuwa Mpina alijiunga na chama tarehe 5 Agosti 2025, nje ya muda rasmi wa kurejesha fomu. Pingamizi hilo lilisababisha Msajili wa Vyama vya Siasa kutengua uteuzi wa Mpina kwa madai ya dosari za kikatiba na kikanuni, hatua iliyozua mtikisiko ndani ya chama.
Hata hivyo, ACT Wazalendo iliwasilisha kesi Mahakama Kuu kupinga maamuzi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kumuondoa Mpina kwenye orodha ya wagombea, ikisema kuwa tume haina mamlaka kisheria ya kumuengua mgombea kwa maelekezo ya Msajili.
Katika maamuzi yake ya hivi karibuni, Mahakama Kuu ya Tanzania kupitia Masijala Kuu Dodoma imeipa Serikali muda wa siku tano pekee kujibu kesi hiyo, baada ya kukataa ombi la kuongezewa siku 14 lililowasilishwa na upande wa Serikali. ACT Wazalendo na Mpina wanadai kuwa INEC ilikiuka Katiba, Sheria na Kanuni za Uchaguzi wakati wa mchakato wa uteuzi wa wagombea Urais uliofanyika Agosti 27, 2025.