Na Theophilida Felician.
Wananchi wanaotumia huduma za tiba asili na tiba mbadala wametakiwa kuwa makini na kuhakikisha wanapata huduma kutoka kwa waganga halali, ili kuepuka madhara makubwa yakiwemo mauaji na uhalifu unaofichwa kwa kivuli cha taaluma hiyo.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Chama cha Waganga wa Tiba Asili Tanzania (TAMESOT), Bw. Lukas Joseph Mlipu, akieleza kuwa kumekuwapo na matukio kadhaa ya ukatili yanayohusiana na watu wanaojitambulisha kama waganga bila kuwa na usajili wala uhalali.
Tukio la Kibaha laibua tahadhari
Akitoa mfano, Mlipu alieleza tukio la hivi karibuni lililotokea katika kitongoji cha Makazi Mapya, wilayani Kibaha mkoani Pwani, ambapo mwananchi Juma Yoram Nyambihira aliuawa na mtu aliyejitambulisha kuwa mganga, anayefahamika kama Ally Juma Shaban.
Baada ya uchunguzi uliofanywa na TAMESOT kupitia Katibu wake wa Mkoa wa Pwani, Ally Masusa Ally, ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo hakuwa mganga wa tiba asili, bali alikuwa akijihusisha na shughuli za ukataji mkaa na kuishi miongoni mwa wananchi akijitambulisha kwa udanganyifu.
Usajili na changamoto za leseni
Mlipu alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutambua waganga waliosajiliwa pekee ndiyo wanaostahili kutoa huduma, na kwamba changamoto kubwa imekuwa ni wavamizi wa taaluma wanaoitumia kama kichaka cha kuendesha uhalifu.
Aidha, aliliomba Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kuweka mazingira rafiki zaidi ya upatikanaji wa leseni kwa waganga, akieleza kuwa malalamiko yamekuwa mengi kutoka kwa baadhi ya waganga ambao walishalipia ada lakini leseni zao hazikutolewa kwa wakati.
Changamoto hizo zimeibua migongano kati ya waganga na wasimamizi wao, mfano ukiwa ni Mkoa wa Kagera, ambapo waganga walieleza malalamiko hayo moja kwa moja mbele ya Katibu Mkuu wa TAMESOT wakati wa ziara ya uhamasishaji wa Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika.
Wito kwa waganga na wananchi
Aidha, aliwataka waganga kote nchini kuhakikisha wanajaza dodoso lililotolewa na baraza la tiba asili, likiwa na lengo la kukusanya maoni yatakayosaidia kuboresha sekta hiyo.
Kwa wananchi, Mlipu alitoa pole kwa familia ya marehemu Nyambihira na kuwasihi kuwa makini wanapotafuta huduma za tiba asili, ili kuepuka kudanganywa na watu wanaochafua taaluma hiyo muhimu kwa jamii.