Mwenyekiti wa Baraza la Biashara na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema jukumu la baraza hilo ni kuhakikisha wanatengeneza mazingira rafiki na wezeshi kwa wafanyabiashara katika Wilaya hiyo.
Ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha Baraza la Biashara la Wilaya kilichofanyika Septemba 12,2025 ambacho kimewakutanisha wadau kutoka taasisi na makundi mbalimbali kutoka ndani ya wilaya ya Ilala.
Amesema wana kila sababu ya kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara kila mwaka ambapo kwa sasa malalamiko ya wafanyabiashara yamepungua sana ukilinganisha na miaka iliyopita.
“Baraza hili ni muhimu na tumekutana makundi mbalimbali hapa na lengo letu kuu ni kuhakikisha wafanyabiashara wanakuwa na mazingira rafiki ya kufanya biashara zao”. Amesema
Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya ambaye pia ni Katibu wa Baraza hilo amesema ushirikiano uliopo kati ya wafanyabiashara na Serikali umewezesha kuongeza ukusanyaji wa mapato katika halmashauri hiyo.
Katika kikao hicho ajenda mbalimbali zilijadiliwa na wajumbe ambapo moja ya ajenda hizo ilikuwa ni kubainisha fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Baraza la Biashara la Wilaya lina jukumu la kujadili mazingira bora ya kufanyia biashara pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara ndogondogo katika wilaya ya Ilala.