Latest Posts

UN YAITAJA TANZANIA KINARA ONGEZEKO LA WATALII

Tanzania imejumuika na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani inayofanyika Septemba 27 kila mwaka, huku imeendelea kutajwa na Shirika la Utalii Duniani kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza Afrika kwa ongezeko kubwa la idadi ya watalii.

Akizungumza  kwenye kilele cha maadhimisho hayo yaliyofanyika katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (picnic site), Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesema ripoti ya UN Tourism ya mwaka 2024 imeitaja Tanzania kuwa kinara barani Afrika katika ongezeko la watalii baada ya janga la UVIKO-19, kwa ukuaji wa asilimia 48, ikifuatiwa na Ethiopia (40%), Morocco (35%), Kenya (11%) na Tunisia (9%).

Dkt. Abbasi amesema ripoti ya mwaka huu (2025) imeionyesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 20 bora duniani zinazofanya vizuri katika sekta ya utalii, kwa wastani wa ukuaji zaidi ya asilimia 50.

“Idadi ya watalii wa kimataifa iliongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 hadi kufikia 2,141,895 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 132.1. Vilevile, watalii wa ndani waliongezeka kutoka 788,933 mwaka 2021 hadi 3,218,352 mwaka 2024, ongezeko la asilimia 307.9. Kwa jumla, hadi Desemba 2024 watalii wa ndani na nje walifikia 5,360,247, sawa na ongezeko la asilimia 107.2,” amesema Dkt. Abbasi.

Aidha, amesema mapato yatokanayo na sekta hiyo yaliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi bilioni 3.9 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 200.

Amefafanua kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020–2025, inayolenga kufikisha watalii milioni 5 na mapato ya dola bilioni 6 ifikapo mwakani. Katika kipindi cha Januari hadi Julai 2025, idadi ya watalii iliongezeka kwa asilimia 9.2, ikifika milioni 1.27 ikilinganishwa na milioni 1.16 mwaka 2024.

Dkt. Abbasi amesema jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, zikiwemo uboreshaji wa miundombinu, matumizi ya TEHAMA, na filamu za The Royal Tour na Amazing Tanzania, zimechangia kuipa nchi nafasi kubwa kimataifa.

Amesema Tanzania pia imeendelea kung’ara kimataifa kwa kutwaa tuzo mbalimbali za utalii za World Travel Awards (WTA) zinazotolewa na World Luxury Media Group Limited.

Dkt. Abbasi amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za utalii kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Utalii ya 1999 na Sheria ya Utalii Sura ya 65, huku akitoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kukuza sekta hiyo muhimu.

Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu: “Utalii na Mabadiliko Endelevu” (Tourism and Sustainable Transformation), ikilenga kuhamasisha ubunifu, taaluma, maendeleo ya biashara na ushirikishwaji wa jamii katika ukuaji wa utalii.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!