Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amewataka Watanzania kuacha kudai maandamano na badala yake kuelekeza nguvu katika kuunga mkono maendeleo ya miundombinu ambayo ndiyo msingi wa kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumza Septemba 28, 2025, mjini Moshi, katika kikao na viongozi na wanachama wa CCM kutoka majimbo ya Vunjo na Moshi Vijijini, Wasira amesema maendeleo ya reli za kisasa na barabara ni nyenzo muhimu za kuleta ustawi wa taifa.
“Wewe unanung’unika tu maandamano, utakula maandamano? Tunataka reli ya kisasa kwa sababu katika dunia inayoendelea, tofauti ya nchi zetu na nchi zilizoendelea ni miundombinu. Ukifika tu unaiona, barabara pana, kuna reli inakwenda speed. Hakuna biashara ya kisasa ya kuuza vitu kwa matenga kichwani, hiyo ni biashara ya zamani. Biashara ya kisasa ni ile inayokwenda haraka sana,” amesema Wasira.
Wasira amebainisha kuwa Ilani ya CCM imepanga kuunganisha maeneo mbalimbali kwa reli ya kisasa, ikiwemo Pugu hadi Musoma kupitia Tanga, Kilimanjaro na Arusha. Amesisitiza kuwa maendeleo ya reli hiyo yatachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana kupitia nafasi mbalimbali zitakazotokana na mradi huo.
“Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inataka reli iunganishe Pugu, Tanga na Arusha kupitia Kilimanjaro. Na sisi Musoma kule, hata isipokuja miaka mitano hii inayokuja mpaka Arusha tunaisubiri. Na ili tuipate, tutahakikisha CCM inaendelea kushinda,” amesema.
Aidha, amesema kuna njia bora na za amani za kufikisha ujumbe bila kuhitaji maandamano, akisisitiza umuhimu wa mshikamano na utulivu wa kitaifa.