Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imeendelea kutoa wito kwa wawekazaji hasa wa ndani kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika maeneo maalum ya uwekezaji ikiwemo eneo la Kwala Industrial Park(KIP) lililopo Kibaha mkoani Pwani.
Eneo la Kwala ni miongoni mwa maeneo manne maalum yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji nchini yakisimamiwa na TISEZA. Eneo hili lina hekari 100 ambazo zote ni kwa ajili ya viwanda.
Maeneo mengine ya uwekezaji ni Bagamoyo mkoani Pwani, Nala mkoani Dodoma na eneo maalum la uwekezaji kwenye sekta ya madini la Buzwagi mkoani Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa Habari Septemba 30, 2025 Kaimu Meneja Habari na Mawasiliano kwa Umma wa TISEZA, Aderina Rushekya amesema eneo la Kwala lina upekee wa kumfanya muwekezaji kuwekeza kwa urahisi ikiwemo uwepo wa miundombinu thabiti ya barabara, uwepo wa reli ya kisasa ya umeme ya SGR ambapo treni ya mizigo inaweza kuchukua na kusafirisha bidhaa na malighafi kutoka viwandani kwa haraka. Reli hii iko takribani mita 100 tu kutoka KIP
Kupitia TISEZA muwekezaji anapohitaji kuwekeza Kwala ni rahisi kwani akifika eneo hilo kuna ofisi ya TISEZA ambayo ni kituo jumuishi cha uwekezaji ‘One Stop Centre’ ambayo muwekezaji ataweza kupewa ushauri, na kupewa huduma zote zinazohitajika ili kuanza kuwekeza ikiwemo BRELLA, TRA, Uhamiaji n.k
Lakini pia muwekezaji anapata bahati ya kupewa ardhi bure ya kujenga kiwanda chake, hii ni kumuondolea ugumu wa kuwaza wapi apate ardhi.
Katika eneo la KIP wapo wawekezaji ambao wanaendelea kujenga viwanda huku wengine wakiwa tayari wameshaanza uzalishaji kama kiwanda cha Snowsea Tanzania Co. Ltd ambacho kinazalisha majokofu.
Kwa mujibu wa Bi. Aderina mwekezaji mzawa anapotaka kuwekeza Kwala vigezo vya msingi ni kuwa ma mtaji wa dola milioni kumi ambayo ni bilioni kumi na mbili na laki tano tu za kitanzania (12,500,000,000/=) huku mwekezaji mgeni akilazimika kuwa na mtaji wa dola milioni kumi sawa na bilioni ishirini na tano tu za kitanzania (25,000,000,000/=).