Latest Posts

BAVICHA WATEMA NYONGO KAWAIDA KUMJIBU RAIS WA TEC

Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) limelipinga vikali kauli zilizotolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa, Mohamed Ally Kawaida, dhidi ya Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa, likisema kauli hizo zimejaa dharau, upotoshaji na kukosa nidhamu.

Tamko hilo limetolewa jijini Dar es Salaam siku ya Jumanne na Naibu Katibu Mkuu wa BAVICHA Tanzania Bara, Revline Albert Mbugi, ambaye amesema CCM imekosa heshima kwa taasisi za dini kwa kumtumia “kijana mdogo asiye na upeo mpana” kumjibu kiongozi wa juu wa TEC.

BAVICHA imesema Kawaida hakunukuu maneno ya Askofu Pisa moja kwa moja na amekuwa kimya kwenye matukio makubwa ya ukiukaji haki nchini. “Ni lini Kawaida amewahi kulaani utekaji wa vijana na watu wengine ambao mpaka leo hawajulikani walipo? Ni lini amezungumza kuhusu risasi zilizomshambulia Tundu Lissu mchana kweupe?” amehoji Mbugi.

 

BAVICHA imewataka vijana nchini kusimama kidete kulinda haki na demokrasia.

“Vijana makini wa nchi hii tunapaswa kusimama bega kwa bega, kudai demokrasia ya kweli na kuikataa dhuluma popote inapojificha,” amesisitiza Mbugi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga Septemba 29, 2025, Kawaida alisema amesikitishwa na matamshi ya Askofu Pisa kuhusu ushiriki wa waumini wa Kanisa Katoliki katika siasa, akidai matamshi hayo yameonesha mgawanyiko badala ya mshikamano.

Hata hivyo, Askofu Pisa, akihutubia Misa ya Jubilee ya miaka 100 ya Seminari Kuu ya Mt. Paulo Mtume Kipalala Septemba 25, 2025, alieleza kuwa kwa mujibu wa sheria za Kanisa Katoliki, viongozi wa Kanisa wakiwemo Mapadri na Watawa hawaruhusiwi kushiriki katika kampeni za kisiasa wala kuhusishwa na chama chochote cha siasa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!