Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Angelina Marco amezindua Soko la Omahe lililopo Kijiji cha Makundusi Kata ya Natta lililojengwa kwa nguvu za wananchi na kugharimu zaidi ya shilingi Milioni 150.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa soko hilo Mhe. Angelina alisema uwepo wa soko katika kijiji cha Makundusi, unaenda kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na kijiji Kwa ujumla kwani wajasiriamali wadogowadogo watapata fursa ya kuuza bidhaa zao na kujipatia kipato huku akiwataka wananchi hao kutunza miundombinu ya soko hilo ili iweze kudumu.
“Niwapongeze Serikali ya kijiji na halmashauri kwa ujumla kwa kubuni mradi huu, kwa kufanya hivi mtawawezesha akina mama wa kijiji hiki kuinuliwa kiuchumi kwani soko hili siyo tu jengo, bali ni kituo cha mabadiliko kitakachoongeza pato la kila mama na kupunguza changamoto ndogo ndogo katika familia zao.
Sambamba na hayo Mhe. Angelina amewesesha kupatikana kwa kiasi cha fedha zaidi ya shilingi Milioni 10 ambayo itatumika kuwapatia mtaji akina mama wa soko hilo na akawataka kuchangamkia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali ya awamu ya sita kupitia Halmashauri pamoja na mikopo ya wajariamali wadogowago.
Kwa upande wao akina mama wa soko hilo, wamepongeza hatua ya ujenzi wa soko hilo na kusema kuwa uwepo wa soko pamoja na kuwa utawaongezea kipato wajasiriamali pia umepunguza changamoto ya kutembea umbali mrefu kununua mahitaji madogo madogo ya familia