Na; mwandishi wetu
Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu imeendelea tena leo, Jumatatu Oktoba 06.2025 kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam chini ya jopo la Majaji watatu (3) wakiongozwa na Jaji Danstan Ndunguru
Kesi hiyo imetajwa Mahakamani hapo leo kwaajili ya mashahidi wa Jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao Mahakamani, na shahidi wa kwanza (1) aliyewasilisha ushahidi wake leo ni ACP George Willbert, Naibu Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, aliyetoa ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Nassor Katuga
ACP George Willbert (48) alianza kwa kuieleza Mahakama kuwa mnamo Aprili 04.2025 Ofisini kwake alifika ASP Kaaya anayefanya kazi kwenye dawati la doria mtandaoni, alipofika alimueleza kuwa aliona picha jongefu kwenye mtandao wa kijamii wa YouTube ya Jambo TV ambapo picha jongefu (Video) hiyo ilibeba kichwa cha habaria kisemacho “Tundu Lissu uso kwa uso na watia nia, No Reforms, No Election”
Anasema ASP Kaaya alimueleza kuwa maudhui yaliyopo kwenye picha hiyo jongefu yalikuwa na ujinai ndani yake, ndipo ASP Kaaya alipochukua simu janja yake na kuanza kumuonesha maudhui hayo ambapo akiwa anaangalia alimuona Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Tundu Lissu akiwa anaongea
Anasema alioneshwa vipande tofauti vya hotuba ya Lissu, ambapo miongoni wa vipande hivyo alimnukuu akisema “Polisi hubeba vibegi mgongoni vyenye kura feki na kwendanavyi kwenye vituo vya kupigia kura”
Wakati ACP George akiendelea kueleza, mshtakiwa Tundu Lissu ambaye anajitetea mwenyewe kwenye kesi hiyo alisimama na kuieleza Mahakama kuwa ushahidi unaohusu Polisi kubeba kura feki kwenye vibegi unaotolewa Mahakama hapo hauhusiani na makosa anayoshtakiwa nayo, Lissu alisema yeye ameshtakiwa kwa kusema “atakinukisha vibaya sana nk”, hivyo kuomba ushahidi huo ufutwe
Wakili wa Serikali Mkuu Nassor Katuga alipinga vikali hoja ya mshtakiwa, kwa kueleza kuwa ni jukumu la Jamhuri kuthibitisha kuhusu mashtaka anayoshtakiwa mtuhumiwa, ambapo baadaye Mahakama ilikubaliana na hoja za Jamhuri na kumruhusu shahidi aendelee kutoa ushahidi wake
ACP George anasema kipande kingine cha video aliyoletewa kilikuwa na maneno yanayosema “Majaji ni watu wa Rais, wengi wao ni Ma-CCM, hupenda kuteuliwa kwenda Mahakama ya Rufani, kwenye Tume na Tume ndio kuna hela, hivyo Mahakamani hakuendeki”
Hoja hiyo ilimuinua Tena na kueleza kuwa hakuna mashtaka yoyote Mahakamani hapo yanayohusu suala la ‘Majaji kuwa Ma-CCM’ hivyo hakubaliani na ushahidi unaotolewa, hata hivyo Mahakama kwa mara nyingine tena ikamweleza mtuhumiwa kuwa mpole kusubiri wakati wake ufike anaweza kuuliza ‘cross examination’
ACP George aliendelea kuieleza Mahakama kuwa, kipande kingine alichokiona kilikuwa na maneno yanayosema “msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli, tunakwenda kuzuia uchaguzi, tunakwenda kuuvuruga kwelikweli, tunakwenda kukinukisha vibaya sana”
Anasema baada ya kuona na kusikiliza vipande hivyo alimwelekeza ASP Michael kufungua majalada mawili ya uchunguzi, jalada la kwanza la uhaini lililopewa namba CDS/IR/727/2025 na jalada la pili ni la kuchapisha taarifa za uwongo mtandaoni lililopewa namba CDS/IR/761/2025
Anasema hatua yake ya pili ilikuwa ni kujiridhisha na uhalali wa video aliyoiona, na hapo akaona ni vyema kuwapata Jambo TV waliorekodi maudhui hayo, huku akiwa tayari ameteua timu ya wapelelezi wa kuchunguza hayo, sambamba na kuwasiliana na Mkuu wa Makosa ya Jinai Mtandaoni DCP Ramadhan Ng’azi aliyekuwa makao makuu ya Jeshi la Polisi Dodoma kumueleza yote hayo, ambapo alitoa ruhusa ya kuendelea na hatua inayofuata
ACP George Willbert anasema baadaye alimpigia simu Kiongozi wa Jambo TV ambapo katika maongezi yao alikiri kuwa video hiyo walirekodi wao lakini akaambiwa kuwa aliyerekodi ni kijana wake (ambaye kwenye kesi hii amepewa jina la ‘P’) na kwamba wakati huo alikuwa Dodoma kikazi
Imeelezwa Mahakamani hapo kuwa, Kiongozi wa Jambo TV alimkabidhi ACP George namba ya ‘P’, ambapo baada ya mawasiliano na maafisa wa Jeshi la Polisi Dodoma, hatimaye ‘P’ alichukuliwa maelezo Doodoma na aliwasilisha video yote ikiwa kwenye card yake
Alipoulizwa kwanini aliwaza kufungua kesi ya uhaini, ACP George anasema maneno yaliyosemwa na mtuhumiwa yamelenga kuitisha serikali kwani uchaguzi mkuu upo kwa mujibu wa Katiba na Sheria, na kwamba Msimamizi wa sheria hizo ni serikali
Pamoja na mambo mengine, ACP George anasema baadaye DCP Ng’azi alimweleza kuhusu askari wa makao makuu ya Polisi Dar es Salaam aliyepangiwa kupeleleza kesi hiyo, na kwamba askari huyo alifika ofisini kwake na kwa pamoja walizungumza kuhusu kesi na hatua ya upelelezi ilipofikia, sambamba na kumkabidhi maafisa wa upelelezi waliokuwa wanaendelea na uchunguzi
ACP George anasema, anakumbuka Oktoba 09.2025 alipigiwa simu na DCP Ng’azi na kujulishwa kwamba mtuhumiwa Tundu Lissu amekamatwa Mbinga mkoani Ruvuma, na kwamba atasafirishwa kutoka huko hadi Dar es Salaam, na ilipofika majira ya Saa 4 asubuhi ya Oktoba 10.2025 mtuhumiwa alifikishwa ofisini kwake na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Ruvuma SSP Charles Mahumbo
Anasema muda mfupi baadaye waliingia watu wanne (4) wanaume Ofisini kwake waliojitambulisha kuwa ni Mawakili wa Tundu Lissu, amewataja watu watu aliowakumbuka kuwa ni pamoja na Dickson Matata, Hekima Mwasipu na Jebra Kambole
Baadaye alimchukua mtuhumiwa na kuelekea kwenye chumba cha faragha kwaajili ya kumchukua maelezo, ambapo hapo aliandika maelezo yake muhimu tu kama vile jina, nafasi yake, umri, kabila, miaka, kazi yake nk lakini mtuhumiwa alisema maelezo mengine yote atayatolea Mahakamani,
Hata hivyo kabla ya kuandika maelezo hayo, mtuhumiwa alipewa nafasi ya kuwa na Wakili, ndugu, jamaa, au rafiki yake wakati wa kuandika maelezo lakini mwenyewe alisema ataandika akiwa peke yake na ilikuwa hivyo
Kesi hiyo imehairishwa hadi kesho, Jumanne Oktoba 07.2025 ambapo mtuhumiwa atakuwa akimuhoji ‘cross examination’ shahidi namba moja (1) wa Jamhuri ACP George Willbert.