Latest Posts

MADEREVA BODABODA NA BAJAJI WATAKIWA KUANZISHA SACCOS ILI KUJIKOMBOA KIUCHUMI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Mhe. Joel Nanauka amewashauri madereva wa bodaboda na bajaji kuwa na umoja imara utakaowawezesha kuanzisha SACCOS itakayowasaidia kupata mitaji yao wenyewe na hivyo kuachana na mikataba migumu isiyo rafiki kwao.

Mhe.Nanauka ametoa ushauri huo kupitia mawasiliano ya simu alipokuwa akizungumza na madereva wa bodaboda na bajaji wa Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara katika hafla fupi iliyoandaliwa na Kampuni ya Twintech inayojishughulisha na uuzaji wa vifaa vya umeme.

Amesema kuwa atatoa ushirikiano na nguvu zake kuhakikisha SACCOS hiyo inafanikiwa ili madereva hao wasilazimike kuingia mikataba migumu ya pikipiki, bali waweze kukopeshana wao kwa wao kwa gharama nafuu lengo ni kuifanya kazi ya bodaboda na bajaji kuwa ya heshima na yenye tija.

Kwa upande wake, Naibu Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Sixmund Lungu amewaasa vijana kutoka makundi mbalimbali, yakiwemo ya waendesha bodaboda na bajaji kutokubali kurubuniwa na watu wachache wasioitakia mema nchi ya Tanzania.

Naye Balozi wa Usalama Barabarani, Nassoro Mansour Nassoro amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu milioni 1.19 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na ajali za barabarani, huku zaidi ya watu milioni 50 wakipata majeraha.

Ameongeza kuwa takwimu za Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini zinaonesha kuwa madereva wa bodaboda wamekuwa miongoni mwa chanzo kikubwa cha ajali hizo, hivyo amewataka kufuata sheria na taratibu za barabarani ili kulinda maisha yao na ya watumiaji wengine wa barabara.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Twintech, Kulwa Issa, amesema ameamua kutoa msaada huo kwa madereva hao kama sehemu ya kurejesha shukrani kwa jamii kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na madereva hao. Pia ametoa msaada kwa kituo cha watoto yatima kinachosimamiwa na Baraza la Wanawake Waislamu Mkoa wa Mtwara, kwa lengo la kuwafariji na kuwasaidia watoto hao.

Nao baadhi ya madereva wa bodaboda na bajaji wamempongeza Mkurugenzi huyo kwa msaada alioutoa pamoja na juhudi na mapambano yake tangu alipoanza safari ya mafanikio.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!