Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe imewaonya wakulima waliopewa mbegu bora za Mbaazi bure na kuwataka kuzipeleka shambani na sio kwenda kuzitumia kama mboga majumbani.
Onyo hilo limetolewa na Theresia Ngoti Afisa Tarafa ya Mawengi wakati wa zoezi la ugawaji wa mbegu za mbaazi uliofanyika katika Kata ya Ludewa.
“Mbegu hizi muende kuzitumia vema na kuzifikisha shambani sio muende kuzipika na kula au kwa matumizi mengine, maafisa ugani nawaasa muweze kushirikiana na wakulima hawa jinsi ya kuzipanda na kusimamia mpaka zinakuwa”amesema Theresia

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa,Wise Mgina amesema halmashauri imejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wananufaika na mpango huo wa ugawaji wa mbegu na kwamba halmashauri hiyo imetenga Milioni 150 kwa ajili ya kununua na kuzalisha mbegu za mazao ya biashara ikiwa ni mkakati wa kuifanya Ludewa kuwa kitovu cha mazao ya chakula na biashara.

Nao baadhi ya wakazi wa Ludewa waliopata mbegu hizo akiwemo Emilia Kayombo na John Kilingile wameshuru serikali kwa kuwashika mkono ambapo wamesema wanaamini watapiga hatua na kuinuka kiuchumi kutokana na mbegu hizo.