Watu zaidi ya 3000 wamepatiwa huduma ya upimaji macho bure pamoja na matibabu katika Hospitali ya Msoga, wilayani Chalinze mkoani Pwani.
Zoezi hilo la siku mbili kuanzia Februari 6 hadi 7, 2026 limehusisha wananchi waliojitokeza Hospitalini hapo kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa kumi jioni.
Huduma hiyo inatolewa na Klabu ya Lions kutoka Jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ikiwa na lengo la kuelimisha na kuhamasisha upimaji wa macho ili kuboresha afya ya macho na kurejesha uwezo wa kuona kwa jamii.
Kwa upande wake, Rais wa Klabu ya Lions Bhumika Shay amesema utunzaji wa macho ni elimu inayotakiwa kuwafikia wananchi kwa ukaribu zaidi ili kuepuka tatizo hilo.

“Ulaji wa vyakula vinavyotunza macho ni muhimu sana ili kulinda afya ya macho, ulaji wa vyakula kama vile mbogamboga na karoti viandaliwe kwa usafi na viliwe kwa mazoea pamoja na kupata muda wa kupumzika na kuwa na mazoea ya upimaji wa macho mara kwa mara kutasaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wacho”, ameeleza.
Akizungumzia zoezi hilo Katibu wa Afya Hospitali ya Msoga, Yasinta Zumba amesema kliniki hiyo ya upimaji wa macho imeambatana na upimaji bure wa magonjwa mbalimbali ikiwemo presha na sukari ambavyo ni miongoni mwa visababishi vya tatizo hilo kwa wengi.
Fauka ya Dokta Elisha Elias Essau Mtaalamu wa macho Hospitali ya Msoga ametoa wito kwa jamii kuacha uvaaji wa miwami ya macho kiholela bila kupima wala kufuata ushauri wa Daktari pamoja na kujenga utamaduni wa kupima macho ili kubaini tatizo hilo mapema.
Wananchi wa wilaya ya Chalinze wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini kwa kuwezesha klabu hiyo kuwapatia matibabu bure.
Nao uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Msoga umeshukuru kwa Lions Club kwa kuchagua wananchi wa Chalinze kuwapatia huduma hii katika zoezi ambalo limetamatika leo Februari 7.