Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa anayekabiliwa na kesi ya uhaini inayoendelea kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam leo, Jumatatu Februari 09.2026 amewaeleza Majaji watatu (3) wanaosikiliza kesi hiyo wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru mambo kadhaa anayoona hatendewi haki akiwa gerezani
Katika maelezo yake, Lissu amelalamikia haki yake ya kuzungumza na Mawakili wake bila kusikilizwa na maafisa wa Magereza, akidai kuwa kwasasa Mawakili wake wakifika gerezani wanapelekwa kwenye chumba cha Mkuu wa Usalama wa gereza, na kwamba wakiwa huko mazungumzo yao yote yanasikilizwa na Mkuu huyo wa usalama, Mkuu wa gereza na maafisa wengine wa Magereza wasiopungua watatu (3)
Amesema kwa mujibu wa kanuni ya 13 ya kanuni za uendeshaji wa Magereza, tangazo la serikali Namba 60 la mwaka 1987, wafungwa au mahabusu wana haki ya kufanya mawasiliano na Mawakili au washauri wao wa kisheria, au mtu yeyote ambaye Afisa wa Magereza anaona anafaa kumwakilisha mfungwa huyo bila kusikilizwa na maafisa wa Magereza, isipokuwa ni kwamba maafisa wa Magereza wanaweza kumuona au kuwaona lakini hawaruhusiwi kuwasikiliza
Amesema jambo hilo si jipya tangu kuanza kwa kesi hiyo, kwani lilianza tangu awali kesi hiyo ikiwa kwenye Mahakama ya ukabidhi (Mahakama ya Hakimu Mkazi -Kisutu, Dar es Salaam) lakini alipoieleza Mahakama wakati huo jambo hilo lilishughulikiwa na halikuwepo tena, hadi liliporejea tena Novemba 12.2025 mara baada ya kesi hiyo kuahirishwa na Mahakama Kuu
Amesema hadi kufikia leo, ni takribani siku 88 sasa tangu kesi hiyo ihairishwe kwa mara ya mwisho Mahakamani hapo, na kwamba muda wote huo hajapata fursa ya kuwasiliana na wanasheria wake, jambo ambalo ni kinyume kabisa na sheria
Tundu Lissu ametoa wito kwa Majaji kuona hatua za kuchukua ili kushughulikia jambo hilo.