Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Mkoani Njombe Zacharia Mwansasu ameagiza kila mwananchi kwenye nyumba yake kuhakikisha amepanda mti ili kutunza mazingira ya Wilaya hiyo.
DC Mwansasu ametoa maelekezo hayo hii leo mara baada ya zoezi la upandaji wa miti ya matunda na vivuli kiwilaya lililofanyika pembezoni mwa barabara kuelekea makao makuu ya halmashauri hiyo.

“Pamoja na kwamba leo tuanapanda miti ya kivuli,lakini kupendezesha barabara zetu ninaomba kila mmoja nyumbani kwake na katika shamba lake katika mwezi huu na kuendelea ahakikishe kwamba ana mti wa matunda,miti ya mbao na ya kupendezesha mazingira”ameagiza DC Mwansasu
Kasimiri David ni mkuu wa kitengo cha mali asili na uhifadhi wa mazingira wa halmashauri hiyo amesema katika zoezi hilo la kuunga mkono jitihada za Rais kunusuru nchi na hali ya jangwa wamefanikiwa kupanda miti zaidi ya 2000.

Kwa upande wake Abdul Mnjokava Askari mwandamizi wa Jeshi la Uhifadhi la Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Wanging’ombe ametoa wito kwa kila mwananchi kuhakikisha anatunza mti ulipandwa katika eneo lake.

Baadhi ya wananchi walioshiriki zoezi hilo akiwemo Haji Kivike pamoja na Oliva Mwita kutoka kitongoji cha Wangama kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kupanda miti kulingana na changamoto za kimazingira ya wilaya hiyo.
