Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita limeiomba Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuona uwezekano wa kuendelea na ukarabati wa barabara zilizoharibika kwa kiasi kikubwa, pamoja na kuweka mifereji ya maji kandokando ya barabara ili kuimarisha miundombinu hiyo, hasa katika kipindi hiki cha mvua.
Wakizungumza nyakati tofauti katika kikao cha baraza hilo, madiwani wameeleza kuwa hali mbaya ya barabara imekuwa ikiwasumbua wananchi, huku baadhi ya maeneo yakishindwa kupitika kabisa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.


Akijibu hoja hizo, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Leonard Bugomola, alitoa ufafanuzi kuhusu bajeti iliyotengwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo. Alieleza kuwa halmashauri imejipanga kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika ipasavyo kuboresha miundombinu ya barabara.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Geita, Bahati Subeya, alisema tayari wamefanya tathmini na kubaini barabara zenye changamoto kubwa, na kwamba wanaendelea na hatua za ukarabati ili kuondoa kero kwa wananchi.
